2015-04-29 08:31:00

Mshikamano wa upendo kwa waathirika wa tetemeko la ardhi Nepal!


Idadi ya watu waliofariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi nchini Nepal na kutikisa pia nchi jirani inaendelea kuongezeka maradufu na kwamba, zoezi la kuwatafuta watu waliofukiwa na kifusi bado linaendelea ka shida na taabu kubwa kutokana na uhaba wa vitendea kazi na hali ngumu ya miundo mbinu kwa ajili ya mawasiliano. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu 4300 wamefariki dunia na kwamba, zaidi ya wananchi millioni moja hawana mahali pa kuishi. Watoto millioni mbili wanahitaji msada wa dharura. Serikali ya Nepal inasema kwamba, zaidi ya majengo 400, 000 yameharibiwa vibaya kutokana na tetemeko la ardhi.

Kutokana na changamoto hizi zote, Baba Mtakatifu Francisko kupitia kwa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum, ametoa awamu ya kwanza ya msaada wa dola laki moja, ili kusaidia mchakato wa huduma nchini Nepal. Fedha hii itapelekwa kwa ajili ya kusaidia juhudi za Kanisa mahalia katika kuwahudumia watu walioathirika kutokana na tetetemeko hili. Hiki ni kielelezo cha mshikamano wa upendo na udugu kwa wananchi wa Nepal ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuyahamasisha Mashirika ya Misaada kimataifa na watu binafsi kuonesha mshikamano wao wa dhati na wananchi wa Nepal.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.