2015-04-28 08:03:00

Wito wa Upadre: Waangalieni na kuwahudumia watu kwa jicho la huruma!


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, hivi karibuni alipokutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na Majandokasisi nchini Cuba anabainaisha kwamba, upungufu, kinzani na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kipadre, si kikwazo katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu.

Changamoto zote hizi ni fursa kwa Wakleri kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa kama walivyofanya wachungaji wanaokumbukwa sana na Mama Kanisa, kama ilivyokuwa kwa Askofu mkuu Adolfo Rodriguez  Herrera aliyefariki dunia kunako mwaka 2003. Anakumbukwa sana kutokana na mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu.

Ni mfano wa wito, maisha na utakatifu wa Mapadre katika utoaji wa huduma kwa Mungu na jirani. Ni kiongozi wa Kanisa aliyejipambanua kwa huduma makini kwa wagonjwa, ndiyo maana Kanisa limeanza mchakato wa kutaka kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri. Ni kielelezo cha Kristo mchungaji mwema, anayeyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Aliwafahamu watu wake, nao wakamfahamu; aliwapenda upeo nao wakamwonjesha upendo wa dhati uliokuwa unabubujika kutoka katika mioyo ya watu walioguswa na huduma ya kichungaji iliyokuwa inatolewa na Mtumishi wa Mungu Askofu mkuu Adolfo Rodriguez Herrera. Huu ni upendo uliomwilishwa katika: wito, maisha na huduma za kichungaji kama Padre na Askofu.

Askofu mkuu Herrera alitekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu, akawa ni Msamaria mwema kwa wagonjwa na wadhambi waliokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa njia ya Kristo na Kanisa lake nchini Cuba. Alionekana kuwa ni kiongozi aliyekita maisha yake katika tafakari ya kina juu ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu, changamoto kwa Mapadre kufanya tafakari ya kina kuhusu huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Huruma ya Mungu.

Kardinali Beniamino Stella anawataka kamwe Wakleri wasikate wala kukatishwa tamaa kutokana na magumu, shida na changamoto wanazokabiliana na zo katika hija ya maisha na utume wao kwa Familia ya Mungu nchini Cuba, bali wajisadake bila ya kujibakiza, tayari kutoka ili kuwaendea wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, tayari kuwatangazia Injili ya Furaha, kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Wakleri wajitaabishe katika Uinjilishaji na kuchoka, ili waweze kupata mapumziko matakatifu, kwa kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, tayari kuchota nguvu ili kusonga mbele katika huduma kwa Familia ya Mungu.

Kardinali Beniamino Stella anawashauri Wakleri pamoja na Majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanajenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Huyu ni Mama wa huruma, kielelezo makini cha upendo katika shughuli na mikakati ya kichungaji. Bikira Maria katika hija ya maisha yake, alijifunza mengi, tangu alipopashwa habari kwamba, atakuwa ni Mama wa Mungu, hadi siku ile ya Ijumaa kuu, alipomsindikiza Mwanaye mpendwa Yesu Kristo katika Njia ya Msalaba, akaonja upendo na huruma ya Kristo kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Bikira Maria ni kielelezo cha mwamini anayemwilisha imani yake katika sala na matendo kwa njia ya ukimya.

Wakleri wanakumbushwa kwamba, upendo katika mikakati na shughuli za kichungaji hauna budi kuwa ni dira na mwongozo wa maisha ya Kipadre. Hapa ni mahali ambapo ufukara, utii na useja wa Kipadre unaonekana na kumwilishwa kama kielelezo cha hali ya juu kabisa katika huduma kwa Familia ya Mungu. Upendo na huruma ya Mungu ni fadhila ambazo zinapaswa kujionesha katika maisha na wito wa Kipadre kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko, ili kutekeleza dhamana ya Uinjilishaji mpya, changamoto kubwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Moyo wa huruma, Ibada na Uchaji wa Mungu ni tunu msingi katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; mahali ambapo Mapadre wanakutana na wadhambi wanaotoka kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kuanza hija ya maisha yanayojikita katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Katika Sakramenti ya Upatanisho, Padre muungamishaji anakutana uso kwa uso na: Ubaya, dhambi na kifo. Mahali hapa panapaswa kuwa ni kiini cha Uinjilishaji mpya, changamoto kubwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubiliei kuu ya huruma ya Mungu.

Hapa Wakleri wanapaswa kuwaangalia Watu wa Mungu kwa jicho la upendo na huruma ya Mungu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake anasema Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, wakati alipokutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na Majandokasisi nchini Cuba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.