Hapa Vatican , Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya elimu ya sayansi,Jumanne 28 Aprili 2015, imekuwa mwenyeji wa warsha muhimu, iliyo chambua kwa kina uhusiano kati ya maadili ya kidini , mabadiliko ya tabia nchi na Maendeleo endelevu, katika lengo la kulinda mazingira ya dunia na kukuza ubinadamu.Kati ya watu mashuhuri walioshiriki katika warsha hii ni Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa , bwana Ban Ki-moon, ambaye hotuba yake, imeitaja Mada mbiu kuu ya warsha kuwa jambo muhimu la kidharura katika nyakati zetu.
Kiongozi huyo wa Kimataifa, ametoa shukurani zake za dhati kwa Papa Francisco na kwa viongozi wa kidini na sayansi, waliofika katika mkutano huu ambamo wameonyesha utambuzi wao katika haja ya kidharura ya kukuza maendeleo endelevu na wakati huohuo, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Na kwamba yeye na Papa Francisco hivi karibuni walipata muda wa kujadili kwa mapana zaidi , masuala mbalimbali yanayoikabili dunia kwa wakati huu.Bwana Ban Ki-Moon ameendelea kusema, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kurekebisha madhara yake ni vipengere muhimu katika kutokomeza umaskini uliokithiri, kupunguza ukosefu wa usawa na usalama sawia sambamba na maendeleo endelevu ya kiuchumi. Na hivyo akaitaja changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi, kuwa tatizo kubwa la nyakati zetu, linalohitaji utendaji makini kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Aliendelea kujali kwamba, mabadiliko ya tabia nchi , pia yana husishwa na afya ya
umma, upatikanaji wa chakula na maji salama, uhamiaji, amani na usalama. Na hivyo
ni suala la kimaadili. Ni suala la haki za kijamii, haki za binadamu na maadili
msingi. Kwa hiyo binadamu anao wajibu msingi katika kulinda na kudumisha mfumo tete
wa mtandao wa maisha ya dunia hii, kwa ajili ya kizazi hiki na vizazi vijavyo. Ndiyo
maana inakuwa ni muhimu sana kwa makundi ya kidini kuwa wazi katika suala hili
na hasa katika mtazamo wa upatanifu wake na sayansi. Katika mabadiliko haya ya tabia
nchi , maoni ya Sayansi na dini hayatofautiani, bali hakika yanapatana.
Kwa maoni hayo Katibu Mkuu Ban , amehimiza wote kwa pamoja, kutoa maelezo bayana
ya kweli, kisayansi na maoni ya kidini , juu ya mabadiliko ya tabia nchi, akisema
sasa si suala la mashaka mashaka bali ni tatizo kubwa na wazi kwamba, mabadiliko
ya tabia nchi yanayotokea sasa , sababu kubwa , ni matendo hasi binadamu . Ukweli
huo, unaozingatiwa sasa na Jopo la Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi na Taasisi
kubwa za kisayansi za kila serikali duniani, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Vatican
ya Elimu ya Sayansi . Na hivyo jibu la Kimataifa kiujumla linatakiwa kutolewa katika
misingi ya uadilifu mzima wa ulimwengu.
Katibu Mkuu Ban Kimoon amesisitiza, mabadiliko ya tabia nchi yaathiri watu wote, ingawa
si katika hali za kulingana. Alieleza kwa kutaja wale ambao, wanakabiliwa na hali
ngumu zaidi , ingawa hawahusiki sana na utendaji mbovu wa binadamu unaosababisha
hali hiyo mbaya , hasa mataifa maskini na watu wanyonge katika jamii . Duniani kote
anasema , kunashuhudiwa jinsi mafuriko, ukame, kupanda kwa viwango vya bahari na dhoruba
vinavyozidi kuongezeka na kusababisha madhara ya kutisha, ikilazimu familia nyingi
kuhamia maeneo mengine , mara nyingi katika hatari kubwa.
Alieleza na kurejea maneno ya Papa Francisco kwamba , dunia inahitaji kuyatazama matatizo
haya kwa jicho la imani, katika uhusiano kati ya mazingira asilia na hadhi ya utu
wa mtu na kwamba walio wanyonge zaidi ni lazima, wawe kiini cha wazo la majadiliano
ya mwaka huu, wakati serikali zinapotafuta jibu la kimataifa katika kukabiliana
na mabadiliko hayo ya tabia nchi na ujengaji wa mfumo mpya kwa ajili ya maendeleo
endelevu.
Katibu Mkuu ameonyesha matumaini yake kwamba, , Malengo mapya ya Maendeleo ya endelevu, yatakayo pitishwa mwezi Septemba, yataweza kuwa na jibu adilifu , lenye kuiweka jamii na mazingira, sambamba na malengo ya kiuchumi, ili kwamba, kutokomeza umaskini uliokithiri, na kusitisha ubaguzi wa kijamii dhidi ya makundi dhaifu na wanyonge, na ulinzi wa mazingira, zinakuwa tunu msingi katika ukamilifu wa mafundisho ya dini zote kuu.
All the contents on this site are copyrighted ©. |