2015-04-28 08:38:00

Mgogoro Mashariki ya Kati: Israeli na Palestina kuzeni majadiliano!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasikitika kusema kwamba, majadiliano kati ya Israeli na Palestina yamekwama na kwamba, Israeli ina haki ya kuwa na uhakika wa usalama wake, lakini usalama huu hauwezi kufikiwa kwa kuwatenga jirani zake. Hapa kuna haja ya kujenga na kuimarisha majadiliano katika misingi ya haki na amani, kwa kutambua uwepo wa mataifa mawili; dhana inayoungwa mkono na Vatican katika sera zake za mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa.

Askofu mkuu Auza anasema, Vatican inapenda kuunganisha sauti yake na wapenda amani kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuanza tena mchakato wa majadiliano ya amani kati ya Palestina na Israeli. Vatican inaihamasisha Serikali ya Lebanon kuanza mchakato utakaoweza kuleta suluhu na hatimaye, kufanikisha uchaguzi mkuu nchini humo, ambao haujafanyika tangu mwezi Mei, 2014. Hapa viongozi wa kisiasa wanapaswa kuweka pembeni masilahi binafsi kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta mafao ya wengi, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Ombwe la ukosefu wa uongozi ni hatari sana kwa Lebanon, ukizingatia hali tete ilivyo huko Mashariki ya Kati. Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaisaidia Lebanon kuwa na amani na utulivu pamoja na kuchangia gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaohifadhiwa nchini humo. Jumuiya ya Kimataifa haina budi pia kuwa macho na makini ili waamini wenye misimamo mikali wasijiingize katika kambi za wakimbizi na wahamiaji na hivyo kusababisha majanga makubwa.

Askofu mkuu Auza anasema, Jumuiya ya Kimataifa inasikitishwa sana na mauaji yanayoendelea kufanywa nchini Syria, kiasi cha kuharibu miundo mbinu kama vile: shule, hospitali, nishati na vyanzo vya maji! Wananchi wa Syria wanakabiliwa na hali ngumu kwa sas ana hata kwa siku za baadaye. Bado kuna dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini; mambo ambayo yanasikitisha sana. Ujumbe wa Vatican unaiomba Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea maisha na haki msingi za wananchi wa Syria, hususan katika mji wa Aleppo ambao kwa sasa umegeuka kuwa ni uwanja wa vita.

Vita, nyanyaso na madhulumu yanayoendelea huko Mashariki ya Kati ni hatari sana kwa uwepo wa Wakristo katika maeneo haya. Uwepo wa tofauti za kidini huko Mashariki ya Kati ni utajiri mkubwa na amana inayopaswa kulindwa na kutetewa kwa kukazia uhuru wa kidini. Kama Jumuiya ya Kimataifa haitakuwa makini, kuna hatari kwamba, Wakristo wakatoweka huko Mashariki ya Kati, jambo ambalo litakuwa ni fedhea kubwa kwa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Umefika wakati anasema Askofu mkuu Auza kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kupinga kwa nguvu zote mauaji ya kinyama yanayofanywa kwa misingi ya kidini na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa haiwezi kuendelea kukaa kimya na kufumbia macho vitendo vya kinyama vinavyofanywa huko Mashariki ya Kati. Kuna umati mkubwa wa watu wanaouwawa, watu wanaolazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao; kuna watu wanaochomwa moto wakiwa hai; kuna watu ambao wanakatwa shingo kwa misingi ya imani. Haya ni mambo ambayo kamwe hayawezi kuvumiliwa yaendelee kutendeka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.