2015-04-28 07:09:00

Changamoto ya wahamiaji haramu: Wekezeni kwenye: amani, elimu na ajira


Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujikita katika misingi ya haki, amani upendo na mshikamano wa dhati, kwa ajili ya kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna haja ya kuwekeza katika sekta ya elimu na uchumi ili kuwawezesha wananchi wengi Barani Afrika kupata fursa za ajira, ili hatimaye, waweze kuondokana na changamoto ya uhamiaji haramu ambao umekuwa ni chanzo cha majanga makubwa kwa wananchi wengi kutoka Barani Afrika, wanaotafuta nafuu ya maisha nje ya Bara la Afrika..

Vijana wengi ambao ni nguvu kazi ya jamii, wanajikuta hawana fursa za ajira na matokeo yake wanaingiwa na kishawishi cha kutaka kukimbilia Barani Ulaya ili kujipatia riziki ya maisha. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Kardinali John Njue, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari hivi karibuni mjini Munich, Ujerumani, tukio ambalo lilikuwa limeandaliwa na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki “Missio Mùnchen”.

Kardinali Njue amekumbuka mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Al Shabaab kwenye Chuo kikuu cha Garissa na kusababisha watu 148 kufariki dunia na wengine wengi kupata majeraha makubwa na kwamba, nusu ya walengwa walikuwa ni Wakristo. Haya ni mauaji yaliyofanywa kwa kisingizio cha misimamo mikali ya kiimani. Tukio hili lilishutumiwa na kulaaniwa na viongozi mbali mbali wa kidini, wakiwemo viongozi wa dini ya Kiislam kutoka Kenya.

Kardinali Njue anasema, kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Al Shabaab mara kwa mara nchini Kenya na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao, Serikali ya Kenya imeutaka Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba, inafunga Kambi ya Wakimbizi ya Dadaab, moja ya kambi kubwa sana duniani zinazotoa hifadhi kwa wakimbizi nchini Kenya. Kardinali Njue anabainisha kwamba, idadi rasmi ya wakimbizi wanaohifadhiwa kambini hapo ni 350, 000. Inahofia kwamba, wapiganaji wa Al Shabaab kutoka Somalia wamejificha kambini hapo.

Kufungwa kwa kambi hii ni kuongeza mateso na nyanyaso dhidi ya watu wasiokuwa na hatia sanjari na kuhatarisha maisha yao, ikiwa kama wananchi hawa watarudishwa tena nchini Somalia, ambako walikimbia vita na mauaji ya kinyama. Ni matumaini ya Kanisa Katoliki nchini Kenya kwamba, kambi hii itaendelea kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Somalia na kuwa kuna majadiliano yanayoendelea kati ya Serikali na Kanisa, ili kuweza kufikia muafaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.