2015-04-27 11:50:00

Tetemeko la ardhi Nepal: Mshikamano wa upendo na udugu unahitajika!


Taarifa ya Jeshi la Polisi kutoka Nepal inaonesha kwamba, hadi sasa kuna watu zaidi ya 3, 617 ambao wamethibitishwa kufariki dunia kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Jumamosi tarehe 26 Aprili 2015 na kutikisa nchi jirani pia. Taarifa zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu 1, 302 kutoka kwenye Bonde la Kathmandu ambao wamefunikwa na kifusi. Zaidi ya watu 6, 515 wamepata majeraha makubwa na kwamba, jitihada za kuwapatia huduma makini bado ni ngumu kutokana uharibifu mkubwa uliofanywa kwenye miundo mbinu. Idadi ya watu waliofariki dunia inatarajiwa kuongezeka maradufu kadiri muda unavyozidi kusonga mbele. Taarifa zinaonesha kwamba, watu 61 wamefariki dunia nchini India kutokana na tetemeko hili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia kwa kuitikia mwaliko wa Baba Mtakatifu Francisko wa kuonesha upendo wa mshikamano, limeamua kuchangia kiasi cha Euro millioni tatu, zitakazosimamiwa na Askofu mkuu Salvatore Pennacchio, Balozi wa Vatican nchini India na Nepal. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka waathirika wa tetemeko hili kwa salam za rambi rambi na mara baada ya sala ya Malkia wa mbingu, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Wakati huo huo, Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa Barani Asia linapenda kutoa salam zao za rambi rambi kwa wote walioguswa na msiba huu mkubwa ndani na nje ya Nepal. Dr. Olav Fykse Tveit anapenda kuungana na wasamaria wema kuwaombea wote waliofariki dunia na kuwatakia faraja wale ambao wamepata majeraha, ili waweze kupona haraka. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayataka Makanisa kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa wananchi wa Nepal walioguswa sana na janga hili zito. Licha ya msaada wa hali na mali, wanahimizwa pia kuwakumbuka na kuwaombea katika sala zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.