2015-04-27 09:23:00

Papa Francisko kurindima wakati wa ufunguzi wa Expo Milano 2015


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe Mosi, Mei 2015 anatarajiwa kufungua Onesho la Chakula Kimataifa mjini Milano, Expo 2015 kwa kuzungumza moja kwa moja kutoka mjini Vatican kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Matangazo haya yanatarajiwa kurushwa moja kwa moja kwa ushirikiano kati ya Kituo cha Televisheni cha Taifa nchini Italia, RAI pamoja na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV.

Uamuzi wa Baba Mtakatifu kushiriki kikamilifu katika onesho hili ni kutambua mchango wa Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, majanga ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Onesho hili linapania kupembua mikakati ya Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na baa la njaa duniani, ili kuhakikisha kwamba, watu wanakuwa na uhakika wa chakula na lishe bora. Kanisa Katoliki linashiriki katika tukio hili kwa njia mbali mbali.

Vatican inashiriki rasmi kwa kuwa na banda lake ambalo linaongozwa na kauli mbiu ”Si mkate peke yake na utupe leo chakula chetu”. Ni banda ambalo linasheheni picha mbali mbali zinazoandamana na tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa chakula katika maisha ya mwanadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Kimsingi, Kanisa linapenda kuishirikisha Jumuiya ya Kimataifa kuangalia umuhimu: Mosi wa kutunza mazingira; Pili: watu kugawana chakula; Tatu: watu kujifunza kuwa na matumizi bora ya chakula; Nne, Chakula kinachowezesha kuona uwepo endelevu wa Mungu duniani. Kwa maneno mengine, dhana inayofumbatwa hapa ni Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini sehemu mbali mbali za dunia. Onesho hili lina mwelekeo mpana zaidi kwani dhana ya chakula inagusa medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: kiroho, kimwili, kitamaduni, kijamii na kiuchumi. Kanisa linashiriki katika onesho hili likijikita zaidi katika masuala ya imani inayomwilishwa kwenye uhalisia wa maisha ya mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.