2015-04-27 08:35:00

Padre ni mhudumu wa Neno la Mungu na Mafumbo ya Kanisa


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Cuba kwa mwaliko wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cuba, amewataka Wakleri kuhakikisha kwamba, wanajitambulisha kama: Mababa wenye huruma na wachungaji wema kuliko kutambulikana kama wafanyakazi na watu wa mshahara. Familia ya Mungu nchini Cuba, inaendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matendo makuu anayoendelea kuwafanyia hususan katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Cuba ni nchi ambayo hata katika udogo wake, imeshuhudia ikitembelewa na Mapapa watatu na kwa sasa kuna cheche za matumaini ya kuanzisha tena uhusiano wa kidplomasia na Marekani, baada ya kusigana kwa miaka zaidi ya hamsini, ambayo imekuwa ni ya shida, taabu na mahangaiko ya wengi, lakini bila ya kukata tamaa, kwani Kanisa limeendelea kuwa bega kwa bega na Familia ya Mungu nchini Cuba. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Beniamino Stella aliwahi kuwa Balozi wa Vatican nchini Cuba kuanzia mwaka 1992 hadi mwaka 1999.

Akizungumza na Wakleri nchini Cuba, Kardinali Stella amewakumbusha kwamba, wanapaswa kuwa ni mfano na kielelezo cha Kristo Mchungaji mwema, kwani wanapaswa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; sadaka inayojionesha katika mchakato wa maisha na utume wa Kipadre, kwa kujikita katika huduma makini kwa Familia ya Mungu wanayoihudumia. Waamini wanatambua na kuthamini sadaka ya maisha ya Wakleri wanaojitosa bila ya kujibakiza; wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa wanaotekeleza dhamana na wito wao katika hali ya unyenyekevu pasi na makuu.

Mara nyingi ni viongozi wanaoonesha dira na njia ya kuafutwa wala si watu wanaotoa amri na kuendelea “kuponda maisha”. Mapadre wanaojisadaka barabara ni mfano mwema katika maisha ya kiroho na wengi wanaweza kuwatambua Mapadre wa namna hii kuwa kweli ni “Watu wa Mungu” ambao hawajamezwa na malimwengu na kutopea huko huko! Cuba ina mifano mingi ya Wakleri waliojisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kristo na Kanisa lake, leo hii ni mifano bora ya kuigwa. Hawa ni kama Mtumishi wa Mungu Padre Felix Varela, Maaskofu Enrique Pèrez Serantes na Askofu Pedro Claro Meurice Estiù.

Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya mtindo na ushuhuda wa maisha yake, anaendelea kujenga na kuimarisha wanafunzi katika shule ya Kristo, kielelezo makini kinachopata chimbuko lake, Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na huduma ya upendo kwa kuwaosha wanafunzi wake miguu, ili kuendeleza dhamana na wito huu kwa Familia ya Mungu. Kardinali Stella amewapatia Watu wa Mungu nchini Cuba salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye anatarajia kutembelea Cuba wakati akiwa njiani kuelekea nchini Marekani, mwezi Septemba 2015.

Katika mahubiri yake, kwa nafasi mbali mbali Kardinali Stella amekazia umuhimu wa wito na maisha ya Kikristo, unaowachangamotisha kutoka katika undani na ubinafsi wao, tayari kuwaendea wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kuwatangazia Injili ya Furaha, Imani na Matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hapa Wakristo wote wanakumbushwa kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki katika Unabii wa Kristo, hivyo wanapaswa kutambua kwamba, wao ni Wamissionari wanaotumwa Kuinjilisha kwa njia ya mifano bora na utakatifu wa maisha.

Kardinali Stella abainisha kwamba, majadiliano ni dhana muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya. Watambue kwamba, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba wanajikita katika majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi. Wawe ni Manabii wa imani, matumaini na mapendo kati ya watu; mashuhuda amini wa furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Kardinali Stella anawataka Wakleri kujenga na kuimarisha mahusiano yao na Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, Fumbo la Utatu Mtakatifu ndio mdau mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji. Wakleri wanapaswa kuambatana na waamini katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kuwashirikisha mang’amuzi ya maisha yao baada ya kukutana na Kristo katika sala, tafakari na maadhimisho mbali mbali ya Mafumbo ya Kanisa.

Wakati huo huo, Baraza la Maaskofu Cuba linabainisha kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo inalenga kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Atasaidia kukoleza mchakato wa Kanisa katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa kwa njia ya majadiliano, kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Cuba kunako mwaka 1998 ilimpokea na kumkaribisha Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako mwaka 2012 Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akawatembelea na kuwaimarisha katika imani na matumaini na mwaka 2015, Papa Francisko anatarajiwa kuwatembelea Mwezi, Septemba, akiwa njiani kuelekea nchini Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.