2015-04-27 15:00:00

Mwaka umepita tangu Yohana XX111 na Yohana Paulo II kutajwa Watakatifu


Mapema Jumatatu hii katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Kardinali  Angelo Sodano , Mkuu wa Dekania ya Makardinali,   aliongoza Ibada ya Misa katika  Madhabahu Kuu ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kwa nia ya kuadhimisha  mwaka mmoja  kupita  tangu Mapapa  Yohana  XXIII  na Yohana Paulo 11 walipotangazwa kuwa Watakatifu. Makardinali wengine walioshiriki katika Ibada hii ni  Kardinali Angelo Comastri, Kardinali  Leonardo Sandri na Kardinali Stanislaw Dziwisz, aliyekuwa amefuatana na ujumbe mkubwa kutoka Krakow Poland.

Kardinali Stanslaw  Dziwisz , akihubiri katika Ibada hii, alimshukuru Kardinali Angelo Sodano , kwa huduma yake  ya wakati alipokuwa Katibu wa Jimbo Takatifu kwa zaidi ya miaka kumi na minne alimotumikia kanisa kama  mshirika wa karibu wa Papa Yohana  Paul II, hadi  ilipofariki  Aprili 2, 2005.  Kardinali Dziwizs , ameonyesha imani yake kwamba,  Kardinali Sodano, bado anaendelea kuwa msaada mkubwa pia kwa Mahalifa wa Petro, na utume wa Kanisa,kwa ujumla. Na kwa namna ya kipekee kwa niaba ya Kanisa la Krakow na raia wa  Poland, alitoa shukurani wale wote  waliochangia kufanikisha maisha matakatifu kwa Yohana Paulo II, na hasa Papa Mstaafu Benedict XVI na Papa Francisco  na pia Mkuu wa Shirika kwa ajili ya utajaji wenye Heri na Watakatifu Kardinali Angelo Amato.

Homilia ya Kardinali Dziwizs, iligeukia pia  masomo ya siku , ikisema katika kumbukumbu hii ya kupita mwaka mmoja tangu watumishi hawa wa Mungu kutajwa Watakatifu, masomo yameongeza furaha na uelewa zaidi katika adhimisho hili , kwa kuwa  yanayoonyesha kupitia jina la wavuvi wa Galilaya, Kristo alichagua na kujenga  msingi wa Kanisa, alimosimika jumuiya kubwa ya wanafunzi wake, ambao leo wanaishi  duniani kote. Kanisa lililoendelea kuchanua tokeo kaburi la Mtakatifu Petro, mfuasi wa kwanza wa Yesu Kristo, aliyemshuhudia Bwana wake ,  katika mji huu wa Roma,  uliokuwa mji  wa kipagani hadi kumwaga damu yake.  Kardinali Dziwisz, alieleza  na kutaja  maneno ya Yesu kwa Petro , Tunza kondoo wangu, akisema , maneno hayo yalimpa  Petro  nguvu mpya ya kumtumikia Bwana wake.

Kardinali aliendelea kuyatazama mazingira ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro akisema, ndani  mwa Kanisa hili mna makaburi ya  waandamizi wengi wa Askofu wa kwanza wa Roma. Na miaka kumi iliyopita, kuliongezeka kaburi jingine la halifa wa Petro aliyelichunga Kanisa  kwa karibia  miaka ishirini na saba, Petro wa miaka yetu, tunayeyajua maisha yake, Yohana Paulo II, anayeitwa kabla  Karol Wojtyla, ambaye wito wa kumtumikia Bwana wake ulioanzia  Wadowice na baadaye  Krakow, kupata ukomavu zaidi alipokabidhiwa kuliongoza Kanisa la Ulimwengu hapo  Oktoba 16, 1978. Hivyo  uzoefu wa Simon Petro ukawa uzoefu wake binafsi. Mahali hapa ambapo Simon Petro, alikuja kutoa ushahidi wake wa hali ya juu, ndivyo ilivyokuwa kwa halifa wake Yohana Paulo II, aliyetaka kuondolewa uhai kwa kupigwa risasi, kutokana na upendo wake kwa Kristo na jirani.. Yohana Paulo  aliyejaliwa busara daima  katika kuonyesha uzoefu wa maisha timilifu, daima alijiweka katika mikono ya Kristo, kwa imani kwamba Kristo alijua udhaifu wake wa kibinadamu. Na hivyo alimpa Kristo nafasi ya kwanza kuyaongoza maisha yake .   Aidha Kardinali alikumbuka siku ambayo Yohana Paulo II alipotangazwa Mwenye Heri na Papa Benedikto XVI,  miaka minne iliyopita, katika Jumapili ya Huruma ya Mungu, akirejea sauti za watu watu wa Mungu zilivyomlilia wakati wa kifo chake, atangazwe Mtakatifu mara moja "Santo subito". Tamko lililoonyesha hamu ya watu wa Mungu kwamba, jina lake lisibaki katika vitabu vya historia ya kanisa tu, lakini aendelee kuongozana wanafunzi wa Yesu,  aliyesulubishwa na kufufuka,  Bwana  wa njia ya imani,  matumaini na upendo katika dunia yetu yenye hofu na mashaka. 

Kardinali Dziwizs anasema , utakatifu  si upendeleo  kwa wanafunzi wachache tu wa Yesu. Utakatifu ni wito kwa watu wote wa taifa la Mungu, kama ilivyosisitizwa na kuwekwa wazi nusu karne iliyopita na Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.  Utakatifu ni kwa  wote wanaomwamini Kristo. Utakatifu haujali cheo au hadhi, lakini wote wameitwa kuishi maisha yenye utimilifu wa Kikristo yaani ukamilifu wa upendo" (Lumen Gentium, 40), wote wameitwa katika  kuwa  Watakatifu  na Yohana Paulo 11, anakuwa ni mfano  hai wa maisha matakatifu yenye  kuwavutia  watu kwa Mungu.  Mtakatifu Yohana Paulo II , alikuwa ni mtu wa maombi, tafakari na mhudumu, aliyeyatolea maisha yake bila kujibakiza kwa ajili ya wengine.  Alimpenda Yesu Kristo kwa upendo Mkuu ,  na  katika upendo huu  aliweza kutoa huduma bila kuchoka kwa Kanisa na kwa dunia. Yeye alifanya kila kitu kwa kila mtu, kwa ajili ya kuifikisha  habari njema katika miisho yote ya dunia.

Kardinali alieleza na kumshukuru Mungu kwa  zawadi hii ya Mtumishi wake  Mtakatifu Yohana Paulo II, ambaye anaendelea kuliiimarisha Kanisa zima hata leo hii. Na hivyo sasa yeye  ni mwombezi wetu mkubwa mbinguni; kwa sababu zetu binafsi, familia na jamii. Kardinali Dziwizs alieleza na kutoa wito kwa watu wote kwama, kumbukumbu hii ya wazi ya Papa Yohana Paulo II katika maisha matakatifu, idumu katika mawazo yetu na katika mioyo yetu, na maisha ya kanisa aliloluhudumia kwa njia tofauti. Na aambatanenasi katika njia yetu ya imani, matumaini na upendo.

Hata hivyo Kardinali pia akatahadharisha kwamba, hatuwezi kuishi tu katika kumbukumbu hizi , lakini inakuwa ni changamoto iliyoko mbele yetu,yenye kugusa mioyo yetu na Kanisa zima na taifa na hasa Kanisa nchini Poland.  Ushahidi wa Yohana Paulo II, unapaswa kushuhudiwa kwa  ndugu zetu na dada zetu ambao bado hawajalijua kanisa , ambao bado hawajajua kuwa  Yesu ni  Bwana na Mwokozi wao. Na aliwataka  Waamini wajichotee urithi wa ujasiri wa Yohana  Paul II, na kutembea nao katika njia ya  maisha ya upendo kwa Mungu na jirani, yaani, kwa njia ya utakatifu. Hiyo ndiyo sala ya muumini kwa maisha yake ya kila siku, sala anayopaswa kuitimiza. 
 

Alikamilisha kwa kutolea  maombi yake  mbele ya Kaburi la Mtakatifu  Petro, Mtakatifu Yohana XXIII na Yohana Paulo II,  pamoja na Mama wa Kristo, mbele ya kiti cha Huruma ya Mungu,  kwa ajili ya kujaliwa zawadi ya imani iliyo hai, tumaini thabiti na mapendo thabiti.








All the contents on this site are copyrighted ©.