2015-04-26 10:53:00

Vijana kiteni maisha yenu katika Umissionari na msikilizeni Roho Mt.


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Mansueto Bianchi, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Vijana Wakatoliki Italia wanaoendesha kongamano la kitaifa linaloongozwa na kauli mbiu “Ukweli unashangaza zaidi kuliko mawazo. Dhamana ya umissionari wa vijana Wakatoliki Italia katika mwanga wa Injili ya Furaha”. Huu ni mwaliko kwa vijana kujikita katika maisha ya kimissionari, kwa kumwachia Roho Mtakatifu atende kazi ndani mwao. Kongamano hili limefunguliwa, Ijumaa tarehe 24 kwa kuwashirikisha wajumbe 700 kutoka katika Majimbo 200 ya Kanisa Katoliki Italia.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka vijana kujichimbia katika maisha na utume wa Kimissionari, ili kuwashirikisha wengine ile harufu nzuri ya huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao. Kipaumbele cha pekee, kiwe ni kwa ajili ya wale wote wanaojisikia kuwa mbali na maisha na utume wa Kanisa; maskini na wale ambao wamesahauliwa na jamii.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Makongamano kama haya yataweza kuasha ndani ya wahusika ari na moyo wa kupenda kusimama kidete, kulinda na kutetea Injili ya Uhai, sanjari na kushiriki katika mchakato unaopania kuleta mageuzi ya kina katika maisha na vipaumbele vya jamii, kwa kuwaelekeza kusimamia mambo mema na matakatifu! Kongamano hili limehudhuriwa pia na Askofu mkuu Savio Hon Tai-Fai, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na viongozi wakuu wa Umoja wa Vijana Wakatoliki Italia.

Vijana wanahamasishwa na Baba Mtakatifu kutoka katika undani wao, ili kwenda pembezoni mwa maisha ya binadamu: kijiografia kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha ya kiroho na kimwili. Lengo kuu la Mama Kanisa ni kukutana na watu wengi zaidi katika medani mbali mbali za maisha, ili kuwatangazia Injili ya Furaha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.