2015-04-26 11:03:00

Tetemeko la ardhi lasababisha maafa makubwa: Nepal, India, Bangaladesh


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za athari za tetemeko la ardhi lililotokea Nepal na kutikisa India, Bangaladesh na Tibet na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu, mali na miundo mbinu. Baba Mtakatifu anapenda kuonesha mshikamano wake wa dhati kwa wote walioguswa na janga hili kubwa na kwamba, anawaombea wote waliopoteza maisha huruma ya Mwenyezi Mungu.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Paul Simick, Msimamizi wa kitume wa Vikarieti ya Nepal. Baba Mtakatifu anawahimiza viongozi wa Serikali na watu wanaotoa msaada kuendeleza juhudi zao ili kuwasaidia watu ambao wameguswa na janga hili. Kwa wote hawa, Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia baraka zake za kitume, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwaponya na kuwafariji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.