2015-04-26 11:15:00

Jubilei ya Huruma ya Mungu: Waonesheni watu uso wa huruma ya Mungu


Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya kwa kushirikiana na wajumbe wa vyama vya Kitume vyenye Ibada kwa Huruma ya Mungu kama ilivyoenezwa na Mtakatifu Faustina Kowalska, wanaendesha Kongamano la Kikanda la Huruma ya Mungu, linalofanyika Kisiwani Sicilia, Kusini wa Italia. Kongamano hili ni muda wa sala na tafakari; muda wa kuabudu na kumshukuru Mungu kwa huruma na mapendo yake kwa binadamu.

Kongamano hili linafanyika katika Jumapili ya Kristo mchungaji mwema, tarehe 26 Aprili 2015, na kuhitimishwa kwa Ibada ya Misa takatifu ambayo inaongozwa na Kardinali Salvatote de Giorgi, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Palermo, Italia. Kwa kutambua umuhimu wa Kongamano hili katika maisha na utume wa Kanisa, hususan wakati huu Mama Kanisa anpoajiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amemwandikia Askofu Rosario Gisana wa Jimbo Katoliki la Piazza Armerina, ujumbe wa matashi mema.

Anawapongeza kwa jitihada hizi za maandalizi yatakayowasaidia waamini kutambua “Uso wa huruma ya Mungu”, tayari kuushuhudia kwa njia ya imani inayomwilishwa katika matendo; kwa njia ya huduma ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ujumbe wa Baba Mtakatifu umeandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kuwapatia baraka zake za kitume pamoja na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.