2015-04-25 10:39:00

Wakristo jitoseni kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa maskini


Mwinjili Marko anapenda kumwonesha Yesu kama sehemu ya mchakato wa hija ya imani iliyofanywa na wafuasi pamoja na mitume wake na hatimaye wakamgundua kuwa kweli Yesu alikuwa ni Mwana wa Mungu. Injili ya Marko inamwonesha Yesu aliyedhalilishwa, aliyeteswa na hata kufa Msalabani. Na kwa njia yake, Kanisa linapenda kuiona ile sura ya Kristo mteswa kati ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni muhtasari katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mwinjili Marko, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Mwinjili Marko kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Venezia ambako Mwinjili Marko ni msimamizi wake; mahali pa sala na tafakari ya Neno la Mungu; lakini pia penye mvuto wa pekee kwa watalii wanaotembelea mji huu ili kushangaa maajabu ya Mungu, mwaliko wa kutunza na kuendeleza mazingira kama ambavyo Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliwahi kushauri, kwani mji wa Venezia ni amana na urithi wa Italia na binadamu wote. Italia ina mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. 

Huu ni mwaliko wa kumfuasa Kristo kwa uaminifu mkubwa katika shule yake ya Injili, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu. Leo hii ushuhuda wa imani sehemu mbali mbali za dunia anasema Kardinali Parolin unaambatana na kifo dini, lakini huruma na upendo wa Mungu unawawezesha wafuasi wa Kristo kuhesabiwa kuwa ni Watakatifu. Mwinjili Marko anawaalika wafuasi wa Kristo kuwa na imani na mapendo thabiti kwa Mwenyezi Mungu pasi na kukata tamaa na changamoto za maisha. 

Injili ya Kristo ni chemchemi ya furaha na nguvu inayowasukuma Wakristo kujitosa katika mchakato wa Uinjilishaji, kwa kushuhudia upendo na huruma ya Mungu, kiini cha maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kugusa akili na mioyo ya watu wengi. Ikumbukwe kwamba, ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake, unajikita katika huruma na unyenyekevu unaojionesha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Umwilisho. Huu ni mwaliko wa kuwaendelea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwatangazia Ukweli wa Injili, toba na wongofu wa ndani. Viongozi katika medani mbali mbali za maisha watoe kipaumbele cha kwanza kwa huduma na mafao ya wengi.

Kardinali Parolin anakumbusha kwamba, tarehe 25 Aprili, 2015, Italia inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu ilipokunja vilago vya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Hata leo hii bado Jumuiya ya Kimataifa imegubikwa na wasi wasi wa vita; mauaji, nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya kidini. Italia inapaswa pia kumshukuru Mungu kwa kuwajalia amani katika kipindi cha miaka 70 iliyopita. Hii ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana katika ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; kwa kukuza mshikamano na udugu kwa maskini na wahamiaji pamoja na kuendelea kuwa macho kwa wanasiasa wanaotaka kuchochea vurugu na kinzani katika jamii badala ya kujenga uhuru na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.