2015-04-25 14:47:00

Jengeni na kudumisha utamaduni wa majadiliano na maridhiano!


Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha kitume cha Wafokolari amewaambia wananchama wa Baraza la Umoja wa Mataifa katika mkutano uliokuwa unajadili umuhimu wa maridhiano na upatanisho kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kukuza na kudumisha majadiliano ya dhati katika ukweli na uwazi dhidi ya utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na mauaji ya kinyama kwa kisingizio cha udini.

Leo hii kuna mamillioni ya watu wanaoendelea kuteseka kwa kulazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao; kuna watu wanauwawa kinyama na wengine kunyanyaswa na kudhulumiwa kwa misingi ya kidini, bila kusahau watu wanaokufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania. Hawa ni wale wanaotoka katika nchi ambazo kuna majanga ya baa la njaa, vita, kinzani na umaskini. Hapa kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ili kukuza maridhiano na upatanisho kati ya watu, kwani haya ni mambo msingi katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Mama Maria Voce alikuwa ni kati ya wawezeshaji kumi na wanne kutoka katika dini mbali mbali, walioshirikisha mawazo yao katika mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa, ili kupata mawazo yatakayoingizwa kwenye ajenda za kufanyiwa kazi mara baada ya kukamilisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ifikapo mwaka 2015. Maridhiano na upatanisho ni kati ya changamoto zinazoikabili Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa mikakati ya ustawi na maendeleo endelevu.

Vita, kinzani, nyanyaso na madhulumu ya kidini ni mambo ambayo kwa kiasi kikubwa yanachangia kuporomoka kwa hatua za maendeleo zilizofikiwa katika sekta ya elimu, uchumi, afya, siasa na kijamii. Hapa kuna haja ya kujenga na kuimarisha utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu. Upatanisho ni dhana muhimu sana katika uundaji wa mwelekeo mpya wa maisha ya mwanadamu, unaoheshimu na kuthamini hata tofauti msingi katika maisha ya mwanadamu kuwa ni utajiri mkubwa wa binadamu. Mwenyezi Mungu amewaumba watu wote sawa, lakini si sawasawa, kuna tofauti kati yao; jambo ambalo ni utajiri mkubwa unaopaswa kuheshimiwa. Watu wakuze utamaduni wa majadiliano, ili kufahamiana badala ya mtindo wa sasa wa kuangaliana kwa jicho la “kengeza”.

Mama Maria Voce anasema amani peke yake ndilo jambo takatifu kwani hii ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliye mwema na mtakatifu. Umoja wa Mataifa unapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Jumuiya ya Kimataifa iheshimu na kuthamini tofauti zilizopo, kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.