2015-04-24 16:47:00

Mwenyeheri Marie Elisabeth Turgeon; Mwanamke wa shoka katika malezi


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, Jumapili, tarehe 26 Aprili 2015, maarufu kama Jumapili ya Kristo mchungaji mwema na siku ya kuombea miito mitakatifu, anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Marie Elisabeth Turgeon, aliyeishi kati ya mwaka 1840 hadi mwaka 1881 kuwa Mwenyeheri. Kardinali Amato anaifanya shughuli hii kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, katika Ibada ya Misa takatifu itakayoadhimishwa kwenye Jimbo la Saint Germain de Rimouski, Canada.

Kardinali Amato anasema baada ya Jimbo la Rimouski kuundwa kwa kumegwa kutoka katika Jimbo kuu la Quèbec, kunako mwaka 1867, Askofu wa kwanza wa Jimbo hili Jean Langevin, alitambua changamoto kubwa ya ujinga uliokuwa unawaelemea watu wake, akaweka mkakati wa elimu kwa wote. Wanawake wa shoka wakajitokeza kuwahudumia vijana wa kizazi kipya wakiwa chini ya usimamizi wa  Elisabeth Turgeon, ambaye alikuwa ni mwanafunzi wake mjini Quèbec. Mwanamke ambaye afya yake daima ilikuwa na mgogoro, lakini Mwenyezi Mungu alimkirimia kipaji cha akili na uwezo mkubwa wa kuongoza.

Mama Elisabeth kama alivyojulikana na wengi, aliishi kwa muda mfupi, akafariki dunia akiwa na umri wa miaka 41, lakini akaacha mambo makubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Ni mwanamke aliyejisadaka kwa ajili ya kutoa elimu Katoliki katika shule maskini na ambazo zilikuwa pembezoni mwa mji. Akawafundisha vijana mambo msingi ya maisha ya Kikristo, kiutu na kimaadili. Katika maisha yake, akajikita katika mambo makuu manne: daima akajitahidi kufahamu na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha; akajisasaka kwa ajili ya kuwaelimisha vijana; akayakita maisha yake katika imani, matumaini na mapendo; daima akijitahidi kujenga na kuimarisha mahusiano na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala.

Hiki ni kielelezo cha imani tendaji, inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kawaida anasema Kardinali Amato, kwa kukazia mambo msingi katika maisha. Mwenyeheri Marie Elizabeth Turgeon alifundwa, akafundika kwenye shule ya Yesu Kristo mchungaji mwema. Shirika la Watawa Mama Yetu wa Rozari Takatifu, wanaweza kuona mfano wa kuigwa kutoka kwa mwanzilishi wao ambaye aliyakita maisha yake katika tafakari na huduma ya mapendo. Ni mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya utume kwa majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya. Huu ni mwaliko wa kuwa ni Wasamaria wema kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.