2015-04-24 16:00:00

Kanisa na Serikali ya Czech kushirikiana zaidi katika elimu, utamaduni


Baba Mtakatifu Francisko siku ya Ijumaa tarehe 24 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na Rais Milos Zeman wa Jamhuri ya Wananchi wa Czech pamoja na ujumbe wake. Baadaye Rais amekutana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili, wamegusia kwa namna ya pekee kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 25 ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Jamhuri ya wananchi wa Czech na Slovachia, uliotiwa sahihi kunako tarehe 19 Aprili 1990. Viongozi hawa wameonesha utashi wa kuendelea kuimarisha mahusiano haya pamoja na kutiliana sahihi mkataba wa makubaliano kati ya nchi hizi mbili.

Kwa pamoja wameonesha pia nia ya Kanisa kuendelea kushirikiana na Serikali kwa karibu zaidi katika maeneo yanayogusa mafao ya wengi zaidi, hususan katika sekta ya elimu, utamaduni na jamii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya taifa zima. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake wamepembua kwa ufupi masuala ya kimataifa hasa zaidi hali ya mateso na mahangaiko ya Wakristo na makundi madogo madogo ya Kiimani huko Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.