2015-04-24 13:37:00

Aprili 25 Siku ya Kimataifa dhidi ya Malaria.


Jumamosi hii 25 Aprili ni Siku ya Kimataifa dhidi ya ugonjwa wa malaria, ambamo  dunia, hutafakari kwa makini zaidi athari za ugonjwa wa malaria, unaosababisha  vifo vingi kila mwaka hasa kwa watoto wadogo. Takwimu za shirika la Afya la Dunia  WHO, zinaonyesha malaria kwa mwaka 2013 iliuawa watu zaidi ya 580,000, wengi wao wakiwa watoto chini ya miaka mitano. Na kwamba ni mtoto mmoja tu kati ya watano barani Afrika waliopata tiba inayofaa kwa mwaka huo 2013. Pamoja na kupungua kwa mashambulio ya vijidudu wa Malaria tangu mwaka  2000, malaria bado ni kitisho kikubwa kwa maisha ya binadamu. 

WHO, katika kuiadhimisha Siku hii dhidi ya ugonjwa wa Malaria,inasema  dunia inapaswa  kutambua haja ya haraka ya kuongeza hatua za kuzuia na uwepo wa ufanisi katika vipimo vya  uchunguzi na matibabu ili kupunguza athari zinazosababishwa na ugonjwa huu, si vifo tu lakini pia katika mtazamo wa uchumi pia.  Hiroki Nakatani ,  mwakilishi wa WHO kwa ajili ya maradhi ya VVU, UKIMWI na malaria, anasema , kwa ajili hii, WHO itachapisha mwongozo mwingine mpya kwa ufupi  kwa ajili ya utoaji wa tiba kwa wagonjwa wa malaria na mapendekezo maalum kuhusu Mambo ya msingi ya kuzuia  ugonjwa huo kwa atoto na wanawake wajawazito.   WHO pia imeandaa mkakati mbinu mpya wa  kimataifa kwa ajili kipindi cha 2016-2030, ambao utajadiliwa mwezi Mei  na Mkutano Mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa, kwa lengo la kupunguza matukio ya ugonjwa wa malaria katika kiwango cha asilimia 40% ifikapo mwaka 2020 na 90% ifikapo mwaka 2030, ikilenga katika mipango ya utendaji kwa  nchi mbalimbali.

Wakati huohuo matokeo ya utafiti yaliyochapishwa katika Jarida la Tiba la Lancet yanaonyesha kwamba ,
chanjo ya malaria iliyotumainiwa kuwa mkombozi kwa adha za malaria, imeonekana kutofanya kazi vizuri kama ilivyotegemewa.  Katika majaribio yaliyofanywa , imeonekana kingo hiyo hufifia baada ya muda. Hata hivyo pamoja na matokeo hayo  mabaya, imetajwa chanjo bado inaweza saidia kukinga  theluthi moja ya watoto wanaopatiwa chanjo kujikinga dhdi ya shambulio la vijidudu wa malaria  kwa muda fulani, wakati watengenezaji wanasonga mbele na hatua za kupata chanjo ya kudumu.  

Juhudi hizi zinafanywa na Kampuni ya dawa ya GlaxoSmithKline ambayo mpaka sasa  katika  utafiti huu,  imetumia mamia ya mamilioni ya dola, kupata uwezekano wa  chanjo ya kupambana na malaria. 

Shirika la Afya Duniani  WHO,  awali liliweka  lengo  la mwaka 2015, chanjo ya malaria iwe imepatikana walau kuweza kutoa kinga ya muda mrefu zaidi  kwa mwaka . Kulingana na utafiti uliochapishwa Ijumaa katika jarida The Lancet, malengo hayo  hajatimizwa , ingawa wanasayansi wanasema, juhudi hizo hazijapotea bure, lakini  ni hatua mbele katika kupata chanjo inafaa.

Utafiti huu ulihusisha watoto 15,500  wakiwemo watoto wachanga  wa barani  Afrika; kundi moja lilipata  dozi tatu, Kundi la pili lilipata dozi moja ya chanjo na baadaye kuongezwa nguvu kidogo na kundi la tatu  hawakupata chanjo hiyo. Lakini watoto wote walitumia kitanda chenye chandarua , na afya yao ilifuatiliwa kwa kipindi cha miaka minne.  Kwa ujumla, matokeo yameonyesha  chanjo  kuwa na ufanisi kwa  asilimia 30 kwa wale waliopata dozi tatu za chanjo, aidha kumekuwa na ahueni katika kundi la pili, lakini kinga hiyo ilionekana kupoteza nguvu kwa kadri siku zilivyokuwa zikipita.

Adrian Hill wa Chuo Kikuu cha Oxford, ambaye anaipinga  chanjo ya  malaria, ametahadharisha kwamba, watoto waliopata dozi tatu katika utafiti  huu ambao hawakuongezewa dawa, pia wanaonekana kuwa dhaifu zaidi  katika shambulio la malaria baadaye.
WHO inatarajia kutoa mapendekezo yake  juu ya chanjo  hii mwezi  Oktoba. 








All the contents on this site are copyrighted ©.