2015-04-23 11:46:00

Mtakatifu George umlinde na kumsimamia Papa Jorge Mario Bergoglio


Mama Kanisa tarehe 23 Aprili anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu George sanjari na kumbu kumbu ya Mtakatifu somo wa Papa Jorge Mario Bergoglio. Mtakatifu George anakumbukwa sana kwa kujifunga kibwebwe kupambana na nguvu za giza kwa watu wa nyakati zake, kama ambavyo Baba Mtakatifu Francisko anavyofanya katika maisha na utume wake. Ni kiongozi anayependa kupandikiza mbegu ya uzuri, wema na utakatifu wa maisha, ili watu wengi waweze kujisikia kuwa kweli ni Watoto wapendwa wa Mungu.

Monsinyo Guillermo Karcher, moja ya wasaidizi wake wa karibu kwa miaka zaidi ya ishirini anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anaonesha ile sura ya Baba mwenye huruma, dhana muhimu sana katika maisha na utume wake kama Padre na Askofu. Hata leo hii, waamini wengi kutoka Argentina wanamkumbuka kama Padre Jorge, hali inayoonesha urafiki, umoja na udugu; mambo msingi sana katika maisha na ustawi wa Kanisa. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wanafarijika wanapokutana na kuzungumza na Papa Francisko, wengi wanapenda kumwita, “Mtu wa watu”.

Anapenda kushirikisha ile Injili ya Furaha kwa watu wanaokabiliana na magumu katika maisha, na kuwatia moyo wale wote wanaoendelea kujisadaka katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Ni mtu wa sala na tafakari anayetaka kutekeleza dhamana na utume wake, kwa kusoma alama za nyakati. Ni kiongozi anayetaka kujenga madaraja ya watu kukutana na kuanzisha mchakato wa umoja, udugu na mshikamano. Adhimisho la Ekaristi Takatifu ni kiini cha maisha na utume wake, ndiyo maana anapenda kuwashirikisha wengine ile Furaha ya Injili, kila siku wakati wa Ibada ya Misa Takatifu.

Wakleri wanapaswa kuonesha ile sura ya Kristo mchungaji mwema kwa kushikamana na Mungu pamoja na watu wanaowahudumia. Baba Mtakatifu anapoadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu somo wake, Familia ya Mungu inamtakia heri na baraka katika maisha na utume wake, aendelee kuwa Mchungaji mwema, mwaminifu, mtakatifu, mkweli na muwazi. Mtakatifu George amlinde na kumsimamia katika mapambano ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inamtakia pia kheri na baraka katika maisha na utume wake kwa maneno yafuatayo "Dominus conservet et vivificet eum"

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.