2015-04-23 07:47:00

Msifumbie macho mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo duniani


Madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia ni dhana inayotishia misingi ya haki, amani, mshikamano na mfungamano wa kimataifa. Jumuiya ya Kimataifa, haiwezi kuendelea kukaa kimya na kufumbia macho mauaji ya kinyama, mateso na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna idadi kubwa ya mashuhuda wanaouwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake katika Karne hii, pengine kuliko ilivyowahi kutokea kwenye Karne zilizopita.

Damu ya Wakristo wasiokuwa na hatia inaendelea kumwagika nchini Iraq, Syria, Nigeria, Libia, Kenya bila kusahau mauaji, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo Barani Asia, mambo yanayoendekezwa na waamini wenye misimamo mikali ya kiimani. Watu wanauwawa kinyama, Makanisa yanalipuliwa; maeneo ya kumbu kumbu za kale yanaharibiwa na watu wanauwawa kwa misingi ya kidini, kama ilivyotokea Garissa, nchini Kenya. Hapa, inaonekana kana kwamba, Wakristo ndio walengwa wakuu wa mauaji, nyanyaso na dhuluma mbali mbali, ingawa hata waamini wa makundi madogo madogo ya kidini nao pia wanadhulumiwa kama inavyojionesha huko Iraq.  Uchunguzi wa kina uliofanywa na kuchapishwa na “Pew Research Center kwa mwaka 2014 unaonesha kwamba, Wakristo wanaongoza kwa kuuwawa, kunyanyaswa na kudhulumiwa kutokana na imani yao, sehemu mbali mbali za dunia.

Huu ni ufafanuzi ambao umetolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati alipokuwa anachangia mada kwenye mkutano wa kimataifa uliokuwa unajadili kuhusu mauaji, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kielelezo tosha kwamba, Umoja wa Mataifa umeshindwa kusimama kidete kulinda na kuwatetea watu wanauwawa na kudhulumiwa kutokana na misingi ya kidini. Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2012, Wakristo wanaoishi katika Nchi 151 kati ya nchi 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, wameuwawa kikatili.

Katika miaka ya hivi karibuni, uhuru wa kidini katika uwanja wa kimataifa umeporomoka kwa kiasi kikubwa, hali inayojionesha kwa namna ya pekee huko Mashariki ya Kati. Wakristo nchini Iraq wanaendelea kupungua kwa kasi ya ajabu kutokana na mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini. Lakini ikumbukwe kwamba, zaidi ya miaka elfu mbili, Wakristo wamekuwa wakiishi huko Mashariki ya Kati, kumbe si haki kuendelea kuwanyanyasa na kuwadhulumu, ili wakimbie kutoka Mashariki ya Kati. Lakini, ikumbukwe kwamba, Mashariki ya Kati pasi na Wakristo ni kuharibu historia ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, kwa kusimama kidete kulinda kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu na maridhiano kati ya watu kwa kukataa kishawishi cha mauaji, dhuluma na nyanyaso kwa misingi ya kidini.

Askofu mkuu Bernadito Auza anasema, kuna haja kwa Umoja wa Mataifa kujifunga kibwebwe kuokoa maisha ya Wakristo huko Mashariki ya Kati, kabla mambo hayaharibika zaidi. Hivi karibuni, katika mkutano wa Baraza la haki msingi za binadamu la Umoja wa Mataifa, nchi wanachama 65, kwa mara ya kwanza wametia sahihi tamko la pamoja kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kuwatetea Wakristo huko Mashariki, dhidi ya mauaji  ya kinyama. Kundi hili linahitaji mshikamano wa dhati, kumbe, ni wakati kwa Umoja wa Mataifa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea bila kuchelewa sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.