2015-04-23 10:32:00

Kardinali Tauran: Wakristo na Waislam: dumisheni majadiliano na udugu


Licha ya matukio mbali mbali yanayoendelea kupamba kurasa za vyombo vya habari kuhusiana na mauaji ya kutisha yanayofanywa dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia, lakini Kanisa litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini ili kujenga na kuimarisha udugu na mshikamano na waamini wa dini ya Kiislam. Ikumbukwe kwamba, chokochoko na madhulumu ya kidini ni mambo yanayofanywa na waamini wachache wa dini ya Kiislam wenye misimamo mikali ya kiimani. Inasikitisha kuona kwamba, dini inatumika kuwa ni chanzo cha mauaji na kinzani za kijamii.

Hii ni sehemu ya tamko lillotolewa na Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, anayewataka waamini wa dini mbali mbali kusimama kidete kujenga, kuimarisha na kudumisha misingi ya haki, amani, udugu na urafiki. Mauaji yanayofanywa kwa misingi ya kidini ni kashfa dhidi ya Mwenyezi Mungu na kielelezo cha kushindwa kwa binadamu. Mauaji na vitendo vya kigaidi vinapaswa kushutumiwa na kulaaniwa na wapenda haki na amani, lakini si haki kuipaka matope dini ya Kiislam, kwani kuna kundi kubwa la waamini wa dini ya Kiislam ambalo halikubaliani kabisa na misimamo mikali ya kidini. Kutokana na changamoto hizi, Kanisa linahamasishwa zaidi kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kuimarisha umoja na mshikamano wa kidugu.

Kardinali Tauran anakumbusha kwamba, waamini wa dini mbali mbali wakiungana pamoja wanaunda nguvu kubwa ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na udugu, ikiwa kama kwa pamoja wataungama na kukiri kwamba, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na pamoja wanaunda Familia kubwa ya Mungu. Waamini wanatambua kwamba, Mungu ni upendo, kumbe, kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, hata pale ambapo mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanaonekana kushika kasi, hizi pia zinaweza kuwa ni dalili za matumaini mapya.

Ili kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na majadiliano ya kidini, kuna haja anasema Kardinali Tauran kuangalia dhamana, maisha na utume wa familia; ni vyema viongozi wa kidini wakawa makini zaidi kwa mafundisho ya dini yanayotolewa kwa watoto na vijana. Familia inapaswa kuhakikisha kwamba, inatekeleza dhamana na wajibu wake kikamilifu, kwani familia ni kitovu na chemchemi ya matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Mauaji yanayotaka kuhalalishwa kwa misingi ya kidini yanapaswa kushutumiwa na kulaaniwa na wapenda amani wote duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.