2015-04-22 14:02:00

Viongozi wa Asia na Afrika watoa wito wa kuunda mfumo mpya wa uchumi duniani


Jumatano hii mjini Jakarta , Viongozi kutoka nchi kadhaa wanachama wa kundi la nchi zisizofungamana na upande wowote, kutoka Asia na Afrika, wameanza mkutano wao, pamoja na mambo mengine, pia kwa ajili ya kumbukumbu ya miaka 60 ya uwepo wa msimamo wa dunia dhidi ya ukoloni,  msimamo ulioongoza katika uwepo wa vita baridi ya nchi zisizofungamana na upande wowote. Katika mazungumzo yao, wametoa wito wa kuwa na dunia iliyo wazi zaidi, katika nguvu za kiuchumi na kuondokana na mawazo ya "kizamani" ya Taasisi za Bretton Woods  yaliyokumbatiwa siku za nyuma.

Rais Robert Mugambe wa Zimbabwe, akishiriki Mkutano huu, amezitaka nchi za Afrika na Asia , kutokumbatia tena masharti ya zamani,  yanayodai kuuza bidhaa ghafi na kuzinunua bidhaa hizo upya baada ya kutengenezwa au  kusindikwa katika nchi za Ulaya, akisema ni mfumo potofu, uliopitwa na wakati.    

Miongoni mwa viongozi walitoa hoja zao ni pamoja na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na Rais wa China Xi Jinping, ambao pia walitarajia kukutana na kutia saini katika  hati ya makubaliano kati ya nchi hizi mbili, kama ishara ya kumaliza upinzani katika mahusiano kati yao .  Taarifa inasema, uhusiano kati ya China na Japan, yamekuwa baridi katika miaka ya hivi karibuni, kwa sababu za migogoro ya tangu wakati wa vita vya zamani  kati ya mataifa haya mawili jirani.  Na kwamba Mazungumzo baina ya nchi mbili mjini  Jakarta  ya Jumatano hii yalitazamiwa kuendelea kuboresha uhusiano  mzuri , ulioanza wakati Abe na Xi walipokutana katika mkutano mjini  Beijing mwishoni mwa mwaka jana.

Rais Xi awali aliuambia mkutano huo kwamba, aina mpya yamahusiano ya kimataifa, yanahitajika  ili kuhimiza ushirikiano kati ya mataifa ya Asia na Afrika, na kwamba nchi zenye viwanda vichache, zina wajibu wa kusaidia nchi zingine katika kundi hilo, bila kuandamana na  masharti ya kisiasa yanayoandamana na hilo, shirika la habari la Xinhua  limeandika.

Rais Indonesian Joko Widodo, kama  mwenyeji wa mkutano huo, amesema wale ambao bado wanasisitiza kwamba matatizo ya kiuchumi duniani  yanaweza tu kutatuliwa kwa njia ya Benki ya Dunia, Shirika la Mfuko wa  Fedha wa dunia na Benki ya Maendeleo ya Asia, hao bado wanang’ang’ania mfumo wa mawazo ya kizamani, ambayo sasa yamepitwa na wakati.  Na hivyo anasema , kuna haja ya kuwa na mabadiliko. Ni muhimu kwamba
 kujenga mfumo mpya wa kimataifa wa kiuchumi , uliowazi zaidi katika nguvu za kiuchumi, kwa kuwa IMF na Benki ya Dunia, viliundwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia na  Marekani na Ulaya kwa mawazo ya Bretton Woods, katika  Mkutano katika New Hampshire katika 1944.  Na sasa mfumo huo umepitwa na wakati.

Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji , Indonesia ilitoa mwaliko kwa wakuu wa nchi na serikali kutoka nchi  109 za Asia na Afrika, lakini ni  viongozi 21, walioweza kuhudhuria mkutano huu. Wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema , hii inaonyesha kwamba, kundi  hili la nchi zisizofungamana na upande wowote, liko katika mwelekeo wa kupoteza nguvu zake,kutokana na mabadiliko makubwa ya kiuchumi duniani. 








All the contents on this site are copyrighted ©.