2015-04-22 09:38:00

Sinodi ya Familia: Changamoto zinazoikabili Injili ya Familia!


Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kutoka Kusini Mashariki mwa Ulaya, hivi karibuni wamehitimisha mkutano wao uliokuwa unafanyika mjini Bucharest, nchini Romania, ili kupembua kwa kina na mapana changamoto za kichungaji katika maisha ya ndoa na familia, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakatoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Ulimwengu mamboleo”.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huu ulikuwa unapania kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kikanisa pamoja na kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji utakowasaidia waamini kusimama kidete kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.  Maaskofu wanasema kwamba, kuna changamoto kubwa katika ndoa mchanganyiko kati ya Wakatoliki na Waorthodox; kwani Makanisa haya mawili yanaiangalia Sakramenti ya Ndoa kwa mwono tofauti, changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, Kanisa linawasaidia wanandoa katika hija ya maisha yao ya imani. Huu unaweza kuwa ni msingi bora wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika uhalisia wa maisha.

Utandawazi wa uchumi kimataifa usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu, umejadiliwa kwa kina na mapana hususan athari zake kwa maisha ya ndoa na familia. Uhamiaji ni changamoto kubwa katika maisha na dhamana ya familia, kwani familia nyingi zimejikuta zikigawanyika kutokana na shughuli za uhamiaji, changamoto kubwa ni kuwasaidia wanandoa kuishi kikamilifu utume wao kwa kuendelea kuwa waaminifu. Wanandoa vijana wanapokuwa ugenini wasaidiwe na Kanisa, ili kuweza kuimarisha maagano na maisha yao ya ndoa.

Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa wanandoa na familia iwalenge wanandoa wenyewe kwa kukuza na kuimarisha mawasiliano, ili kuzisaidia familia kuwa kweli hai, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia. Wanafamilia waoneshwe mshikamano wa dhati wakati wa raha na shida katika safari ya maisha yao ya ndoa. Utume wa familia unaoendeshwa na vyama vya kitume ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha Injili ya Familia. Wanachama wa vyama hivi wasaidiwe kupata majiundo makini ili kuweza kumwilisha karama katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu kwa namna ya pekee, wanawahimiza wanandoa kushiriki kikamilifu katika maisha ya Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Upatanisho; ili kujichotea utajiri wa Neno la Mungu na chakula cha njiani, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Familia; pale ambapo Kristo atakuwa yote katika yote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.