2015-04-22 07:03:00

Boko Haram: Kinashamiri kutokana na umaskini na ujinga wa watu!


Rais mteule Muhammadu Buhari wa Nigeria anasema, Serikali yake mpya inataka kutoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa elimu kama njia ya kupambana na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ambacho kimekuwa ni tishio kwa maisha na usalama wa wananchi ndani na nje ya Nigeria. Rais Buhari anayetarajiwa kuapishwa na kuanza kushika madaraka rasmi hapo tarehe 29 Mei 2015 anasema kwamba, mapambano dhidi ya Boko Haram yanapaswa kujikita katika mbinu mkakati wa kijeshi sanjari na elimu makini kwa vijana, ili kuwasaidia kutambua madhara yanayosababishwa na vitendo vya kigaidi. Kutokana na umaskini na ujinga anasema Rais Buhari, vijana wengi wanajikuta wakitumbukizwa na hatimaye, kujiunga na vitendo vya kigaidi, wakiwa na matumaini ya kupata pengine utajiri wa haraka haraka bila kuhesababu madhara yake kwa jamii husika.

Rais Buhari anasema, Serikali ya Rais Goodluck Jonathan aliyeshindwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini Nigeria, alidharau uwezo wa Boko Haram na kutolivalia njuga tatizo la maafa yaliyokuwa yanasababishwa na Boko Haram. Mwaka mzima umepita tangu wasichana wa shule ya Sekondari ya Chibok walipotekwa nyara na hawajulikani mahali walipo.

Swali la msingi ambalo wananchi wa Nigeria wanapaswa kujiuliza anasema Rais Buhari, ni kwa nini kuna kundi kubwa la vijana wanaojiunga na Boko Haram licha ya kufahamu madhara na hatari zinazoweza kuwakabili kwa uamuzi kama huo? Tatizo kubwa hapa anasema Rais mteule ni umaskini na ujinga. Nigeria haina budi kuwekeza katika elimu makini, ili kuwasaidia watu kupambana na mazingira yao, ili kuyafanya yawe bora zaidi. Mzee Nelson Mandela aliwahi kusema kwamba, elimu ni silaha madhubuti katika kuleta mageuzi duniani. Rais mteule Buhari ameyasema haya wakati wa mahoniano maalum na Jarida la “Jeune Afrique” na “International New York Times”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.