2015-04-21 09:52:00

Wanawake fanyeni mageuzi yanayojikita katika utu wema kwa wasichana


Viongozi wa Wanawake Wakatoliki Kimataifa wanaotoa huduma kwa wasichana, hivi karibuni wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewahamasisha kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mageuzi yanayolenga kudumisha utu wema miongoni mwa wasichana. Hili ni kundi la wanawake linalotekeleza dhamana na utume wake katika mazingira magumu na hatarishi. Kuna ongezeko kubwa la umaskini duniani, hali ambayo inahitaji mipango madhubuti ili kuweza kukabiliana na changamoto za maisha, katika huduma kwa wasichana: kiroho na kimwili, huduma ambayo inapaswa kujikita katika furaha, kama alivyofanya Yesu mwenyewe.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, kutokana na changamoto za uhamiaji, kuna haja kwa wanawake hawa kusimama kidete katika huduma na ukarimu kwa zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu, kama kielelezo cha imani tendaji. Wanawake hawa kwanza kabisa wajenge na kuimarisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuweza kujenga imani na matumaini katika malezi na makuzi yao: kiroho na kimwili. Wasaidiwe kufahamu tunu msingi za maisha ya Kiinjili, kwa njia ya ushuhuda unaotolewa na huduma ya wanawake hawa, ili wao pia waweze kuwa ni vyombo vya furaha.

Wanawake pia waoneshe ujasiri wa kujifunza kutoka kwa wasichana wanaowahudumia, kwani mara nyingi wamekuwa ni vielelezo vya udugu na mshikamano na kwamba, kutokana na udhaifu wao, wamekuwa ni watu ambao wanamtegemea zaidi Mwenyezi Mungu. Wanawake wajenge moyo wa kuwa ni mitume na wamissionari, ili waweze kufariji, kuokoa na kuwasindikiza wasichana katika safari yao ya maisha. Baba Mtakatifu anawahamasisha wanawake kuendelea kutangaza Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Huduma yao makini ni ushuhuda wa Kristo ambaye alionesha upendeleo wa pekee kwa maskini na wanyonge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.