2015-04-21 06:58:00

Maaskofu Katoliki Gabon: Kanisa kuendelea kuwekeza katika majiundo!


Askofu Mathieu Madega Lebouakehan wa Jimbo Katoliki Mouila, Gabon anabainisha kwamba,  changamoto zinazolikabili Kanisa nchini Gabon zinatokana na maisha na utume wa Kanisa unaopaswa kuzamisha mizizi yake katika maisha na vipaumbele vya waamini kwa kuwa na katekesi makini na endelevu inayoweza kuwasaidia waamini kuwa kweli ni mashuhuda amini wa Kristo na Kanisa lake.

Kanisa lina matumaini makubwa kwa sasa na kwa siku za usoni kutokana na kuongezeka kwa miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Kwa sasa kuna idadi kubwa ya vijana wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo, Kanisa na jirani zao katika maisha ya kipadre na kitawa. Lakini pia kuna kundi kubwa la vijana wanaoamua kufunga ndoa za Kikristo, tayari kuanza hija ya kutakatifuzana kama Bwana na Bibi, huku wakijitahidi kujenga familia, ambayo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Kanisa linaendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene katika misingi ya haki, amani, ukweli na uwazi, ili kushiriki kikamilifu katika huduma kwa Familia ya Mungu nchini Gabon. Lengo kuu ni kusimamia haki msingi za binadamu, utu na heshima yake, kwani ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hadi sasa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali wanaishi kwa amani kama ndugu na wala tofauti zao za kidini si shida inayowajengea kinzani na utengano, bali ni mafuta na baraka katika maisha ya wananchi wengi wa Gabon.

Katika miaka ya hivi karibuni, Gabon imejikuta ikichechemea katika sekta ya uchumi kutokana na kuporomoka kwa bei ya nishati ya mafuta katika soko la kimataifa na matokeo yake, kumekuwepo na migomo katika sekta mbali mbali za maisha na huduma nchini humo. Kumekuwepo na upunguzaji wa wafanyakazi katika sekta ya umma hali ambayo ina madhara makubwa katika maisha ya familia nyingi nchini Gabon.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.