2015-04-21 12:12:00

Bado kuna akina Stefano Shahidi wanaopigwa mawe kwa ajili ya imani yao


Hata leo hii kuna watu wanaoendelea: kunyanyaswa, kudhulumiwa na kusulubiwa kwa kupigwa mawe kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Stefano Shahidi aliyesimama kidete kutangaza imani kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu! Hawa ni mashuhuda wa imani kwa nyakati hizi, wanaoendelea kuandika historia ya Kanisa kwa njia ya damu yao inayomwagika sehemu mbali mbali za dunia, kama ilivyokuwa kwa Kanisa la mwanzo. Ni mashuhuda wanaoshibishwa kwa mkate ulioshuka kutoka mbinguni, unaowapatia jeuri ya kuvumilia mateso na  mahangaiko katika maisha.

Neno la Mungu linagonga mwamba kwenye mioyo migumu, isiyokubali kutubu na kumwongokea Mungu. Hawa ni watu ambao wanashindwa kutambua hekima ya Mungu katika maisha yao, wanataka kuupindisha ukweli kwa kutoa mashuhuda wa uongo ambao kamwe hawawezi kufua dafu kwa hekima inayobubujika kutoka kwa Mtakatifu Stefano Shahidi wa Neno la Mungu na Kristo Mfufuka.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 21 Aprili 2015. Baba Mtakatifu anasema, Neno la Mungu ni kama upanga wenye makali kuwili, unakata mioyo ya watu. Kuna Wakristo wengi ambao wameuwawa kwa vile walikuwa waaminifu kwa Neno na ukweli wa Kimungu. Kuna mashahidi wengi wanaoendelea kusulubishwa sehemu mbali mbali za dunia kama ilivyokuwa kwa Stefano Shahidi, kwa kudhani kwamba, kwa njia ya mauaji, dhuluma na mateso wanatekeleza mapenzi ya Mungu kadiri ya imani yao.

Ikumbukwe kwamba, historia ya kweli ya Mama Kanisa limeandikwa kwa damu ya mashuhuda wa imani na ukweli wa Kimungu. Hawa ni kama Wakristo waliouwawa hivi karibuni nchini Lybia; wahamiaji waliozamishwa majini kwa vile tu walikuwa ni Wakristo. Kanisa kwa nyakati hizi linajipambanua kuwa ni Kanisa la mashuhuda wa imani na kwa njia ya mateso na ushuhuda wao, Kanisa linapata baraka na neema ya kusonga mbele. Wakristo wanaendelea kuhukumiwa na wakuu wa mabaraza wanaodhani kwamba, wanakumbatia ukweli! Kuna Wakristo ambao wanaendelea kuwa kweli  nimashuhuda wa Kristo na Kanisa lake, hata wakiwa ndani ya familia zao, lakini Yesu ndiye Mkate unaozima kiu na njaa ya watu wake wanaonyanyasika na kudhulumiwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.