2015-04-20 12:15:00

Wafiadini na watakatifu ni mfano bora unaoonesha nguvu ya imani


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu tarehe 20 Aprili 2015, ameelezea umuhimu wa wafiadini wanavyowasaidia waamini kuondokana na kishawishi cha kugeuza imani kuwa ni silaha kwa ajili ya mafao binafsi, kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha na utume wa Yesu. Baada ya kula na kushiba, baadhi ya watu walitaka kujinufaisha wenyewe kwa kutumia nguvu za miujiza zilizooneshwa na Yesu. Mwelekeo huu potofu anasema Baba Mtakatifu unajionesha katika sehemu mbali mbali za Maandiko Matakatifu.

Mama yake watoto wa Mzee Zebedayo alitaka watoto wake wapate upendeleo wa pekee katika Ufalme waYesu, kwa kuwa na madaraka na kusahau kwamba, walikuwa wameteuliwa na Yesu ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu; wafungwa kufunguliwa kwao, vipofu kuweza kuona tena na kusetwa kwa waliokandamizwa. Mitume wanatumwa kutangaza Mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Waamini wanapaswa kuachana na unafiki na hivyo kuanza kujikita katika uhalisia maisha na utume wa Kristo.

Kishawishi cha kutaka madaraka kilijionesha pia wakati Yesu alipokuwa Jangwani kwa muda wa siku arobaini; Shetani alimtaka Yesu kumwabudu; kishawishi ambacho kimeendelea kuliandama Kanisa na watoto wake wote. Hiki ni kishawishi kinachowaelekeza waamini kumezwa na malimwengu na kuendelea kuonesha unafiki wa kumfuasa Kristo. Kumbe, Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni mashuhuda wa Yesu kwa maneno na matendo yao, daima wakiwa na imani thabiti pasi na kuyumbishwa na malimwengu.

Mwenyezi Mungu kwa njia ya ushuhuda wa wafiadini na watakatifu, anawaonesha utakatifu wa maisha unaofumbatwa kwa kumfuasa Yesu Kristo; kwa kutambua na kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa Mbinguni sanjari na kuamini kwamba, Yesu Kristo ndiye aliyetumwa na Baba yake wa mbinguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.