2015-04-20 15:38:00

Maaskofu Gabon: Simameni kidete kutetea Injili ya Uhai, Umoja na Udugu


Baba Mtakatifu Francisko analitaka Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai; kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa; sanjari na kujitahidi kuwaonesha vijana ile Sura ya huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku. Amewataka vijana kuwa madhubuti katika imani yao na kamwe wasikubali kuyumbishwa kama “daladala” iliyokatika usukani, wala kumezwa na malimwengu.

Baba Mtakatifu ameyasema haya Jumatatu, tarehe 20 Aprili 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na Maaskofu Katoliki Gabon ambao kwa sasa wako mjini Roma katika hija yao ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Baba Mtakatifu anawakumbusha Maaskofu kwamba,  Kanisa ni Familia ya Mungu inayowajibika kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika misingi ya haki, amani, furaha. Injili inawaokoa waamini kutoka katika nguvu za giza na kuwaelekeza kwenye Ufalme wa Mungu; ambao Gabon inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 170 tangu Ukristo ulipoingia nchini humo.

Hii ni dhamana iliyotekelezwa na Wamissionari waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake na kupokelewa na mashuhuda wa imani kutoka Gabon, kiasi cha kujenga umoja na udugu unaovuka mipaka ya ukabila na utengano kati ya watu. Umoja na mshikamano, unaliwezesha Kanisa kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi; tayari kusimama kidete katika urika wao kama Maaskofu ili kutetea na kudumisha mafao na ustawi wa wengi. Kanisa linahamasishwa kujifunga kibwebwe katika mchakato wa ujenzi wa dunia ambamo haki na udugu vinakuzwa na kudumishwa.

Baba Mtakatifu anapongeza jitihada zinazofanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon katika kukuza mchakato wa majadiliano ya kidini kwa kuanzisha kituo maalum cha Mafundisho Jamii ya Kanisa na Majadiliano ya Kidini, kunako mwaka 2011. Anawataka Maaskofu kuwa ni sauti ya wanyonge kwa kutetea utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu; kwa kujikita katika huduma bora zinazotolewa katika medani mbali mbali za maisha, hususan katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii; daima wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko anawahimiza Maaskofu wa Gabon kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha: majadiliano, umoja na udugu miongoni mwa Wakleri, kama sehemu ya maisha na utume wao. Maaskofu pale inapofaa wawajibishe Mapadre wao kwa kuzingatia haki na upendo. Maaskofu wawasaidie vijana wanaotaka kujitosa kumtumikia Mungu na jirani zao kwa njia ya wito wa kipadre na maisha ya kitawa. Wahakikishe kwamba, wanawapatia majiundo makini yanayojikita katika Injili ya Kristo, kanuni maadili na tunu bora za maisha ya kiafrika; kwa kutambua kwamba, kwa namna ya pekee wanahamasishwa kuwa wakweli na watu wanaowajibika mbele ya Mungu na Jamii inayowazunguka.

Baba Mtakatifu anasema katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, kuna haja kwa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majadiliano ya kina na watawa wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume; ili kukuza na kudumisha maisha na utume wa Kanisa. Wawashirikishe waamini walei katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya utume wa Kanisa. Maaskofu watambue kwamba, kimsingi, Kanisa ni la kimissionari, kumbe, majiundo makini ya walei hayana budi kugusa tunu msingi za maisha ya kiutu na Kikristo; ili kweli waamini hao waweze kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa Uinjilishaji na maendeleo endelevu, kwa kuwaendelea wale wanaoishi pembezoni mwa jamii,  ili kuwaonjesha Injili ya Furaha.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuwasaidia vijana kuona ukweli wa maisha na kamwe wasiogelee katika ombwe na mawazo ya kufikirika. Maaskofu wajitahidi kuwaonesha vijana Sura ya Kristo, ambaye ni rafiki na kiongozi wa vijana. Vijana washikamane na Kristo ili kushinda kishawishi cha kutanga tanga kwenye misingi ya imani na matokeo yake wanajikuta wakiwa wamemezwa na malimwengu. Vijana washinde kishawishi cha kutaka maisha ya mkato kwa kujitafutia utajiri wa haraka haraka, kwani madhara yake yanajionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya familia. Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakuwa ni fursa ya kuweza kuwajengea waamini uwezo wa kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.