2015-04-20 07:43:00

Jubilee ya miaka 25 ya Mfuko wa Papa: Majiundo na maendeleo endelevu


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 17 Aprili 2015 amekutana na kuzungumza na wanachama wa Mfuko wa Papa ambao katika kipindi cha miaka ishirini na mitano, umejikita kwa namna ya pekee katika mchakato wa majiundo makini wa mihimili ya Uinjilishaji sanjari na maendeleo endelevu ya binadamu. Baba Mtakatifu anaendelea kuwahimiza wajumbe hawa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Anawashukuru kwa huduma makini ambayo wanaendelea kuitoa kwa ajili ya kusaidia majiundo makini kwa Wakleri sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Donald William Wuerl, Rais wa Mfuko wa Papa, wakati wa hija ya wanachama wa Mfuko huu mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 25, anasema, kwa hakika wameendelea kushikamana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake kwa Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu ni kielelezo cha huduma ya upendo, inayofumbatwa katika mahitaji msingi ya binadamu, kama anavyobainisha Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Injili ya Furaha, Evangelii gaudium.

Huduma ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Donald William Wuerl wakati walipokutana na Baba Mtakatifu Francisko wamewakilisha miradi 130 itakayogharimu kiasi cha dolla za kimarekani millioni 14. Hapa Mfuko wa Papa unatoa pia kiasi cha dolla 600, 000 kwa ajili ya kusaidia majiundo makini ya Wakleri, Watawa na Walei wanaosoma kwenye vyuo mbali mbali vya Kipapa hapa Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.