2015-04-20 08:29:00

Jubilee ya Huruma ya Mungu: Dhana ya huruma ya Mungu


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu, tumsifu Yesu Kristo. Karibu katika kipindi hiki ambapo kwa wakati huu, tutaahirisha kwa muda tafakari yetu juu ya Mafundisho ya imani yetu kama yanavyomwilishwa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, na badala yake; ili kufikiri na kwenda pamoja na Kanisa, tutajikita katika kuufafanua Waraka wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya maadhimisho ya mwaka wa Huruma ya Mungu, waraka ujulikanao kwa lugha ya Kilatini Misericordiae vultus, yaani Uso wa Huruma au Sura ya Huruma.

Tunafanya hivi mpendwa msikilizaji, ili kukuweka tayari kiakili, kimwili, kiroho na kisaikolojia na kiutashi, ili utakapofika wakati wa kuuzindua rasmi mwaka huo wa Jubilei ya Huruma ya Mungu  hapo tarehe 8 Desemba 2015; sote tuwe tunafahamu kwa kina, Kanisa linadhamiria nini katika Jubilee hiyo ya Huruma ya Mungu. Tutaufafanua waraka huu kama ulivyoandikwa na Baba Mtakatifu Francisko. Ni barua ya kitume.

Baba Mtakatifiu anaianza barua hii kwa kuielezea huruma ya Mungu kama inavyojimwilisha katika Kristo. Anasema, Yesu Kristo ndiye uso wa Huruma ya Baba. Huruma hiyo ya Baba wa milele inadhihirika an kufikia utimilifu wa juu katika Yesu wa Nazareti. Baba aliye mwingi wa huruma (Ef. 2:14), aliyejidhihirisha kwa Musa kama Mungu wa huruma na neema, asiye mwepesi wa harissa na mwingi wa upendo na fadhili (Kut. 34:6), nyakati zote hajaacha kuonesha asili yake ya kimungu.

Wakati ulipotimia, kila kitu kilipokuwa kimepangwa kadiri ya mpango wake wa ukombozi, alimtuma mwanawe wa pekee ulimwenguni, akazaliwa na Bikira Maria, ili kuudhihirisha upendo wake kwetu katika ukamilifu wote. Kristo mwenyewe anasema, yeyote aliyeniona mimi, amemwona Baba (Yoh 14:9). Yesu wa Nazareti, kwa nameno yake, kwa matendo yake na nafsi yake nzima, vinadhihirisha huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anaendele kutualika sisi sote kutafakari daima huruma ya Mungu. Ni chemchemi ya furaha, utulivu  na amani. Wokovu wetu unategemea huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema: huruma ni neno linalodhihirisha fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma: ni tendo la mwisho na la juu kabisa ambalo kwalo Mungu anakuja kukutana nasi. Huruma ni sheria-msingi iliyomo katika moyo wa kila mtu anayewatazama kwa wema binadamu wenzake anaokutana nao  katika mapito ya maisha. Huruma: ni daraja inayomuunganisha Mungu na  mwanadamu, na inaelekeza mioyo yetu kwenye tumaini la kupendwa daima licha ya udhambi wetu.

Daima tunaalikwa kuitazama huruma kwa umakini zaidi, ili tuweze kuwa alama wazi za matendo ya Mungu katika maisha yetu. Ni kwa sababu hii, anasema Baba Mtakatifu, nimetangaza Jubilee ya pekee ya Huruma, kama nafasi ya pekee kwa Kanisa; wakati ambamo ushuhuda wa waamini unaweza kukua na kuimarika zaidi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema,  katika mwaka huu wa Huruma ya Mungu, tutamkabidhi Kristo Yesu maisha ya Kanisa, wanadamu wote na ulimwengu mzima kwa ujumla. Tutamwomba Kristo atumiminie wingi wa huruma yake kama umande wa asubuhi ili sote kwa pamoja tujenge kesho iliyo angavu zaidi.  Anatamani Baba Mtakatifu kwamba mwaka huo ujao  uzamishwe katika huruma ili tuweze kutoka kuwaendea binadamu wote na kuwapelekea habari njema na upendo wa Mungu. Mwangwi wa huruma umfikie kila mmoja; wote wanaoamini na wale walio mbali, kama alama ya kwamba Ufalme wa Mungu upo tayari kati yetu.

Mungu amedhihirisha ukuu wake kwa njia ya huruma yake, kama anavyotufundisha Mt. Tomaso wa Akwino, akisema, huruma sio alama ya udhaifu, bali ni alama ya ujasiri na ukuu.  Tukielekeza macho yetu kwa Yesu na tazama yake ya huruma, tunaona upendo wa utatu Mtakatifu. Utume wa Yesu  alioupokea kutoka kwa Baba, ulikuwa ni kulidhihirisha fumbo la upendo huu  katika ukamilifu wote. Mungu ni Upendo. Upendo huu umedhihirishwa  kwa wazi zaidi na unagusika katika maisha mazima ya Yesu. Nafsi yake ni Upendo unaofafanuliwa katika huruma yake kuu. Ishara anazotenda, kwa namna ya pekee kwa wadhambi, masikini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wagonjwa, wanaoteseka, katika hayo yote alilenga kutufundisha huruma. Kila kitu ndani mwake kinaongelea huruma.

Mpendwa Msikilizaji; Lengo letu: Tufikiri pamoja na Kanisa – twende pamoja. Jubilee  ya Mwaka wa Huruma ya Mungu tutakayoiadhimisha, inatutafakarisha sisi wenyewe kila mmoja wetu jinsi alivyoweza kupokea huruma ya Mungu katika maisha. Hata kama umesahau, ipo siku uliguswa na huruma ya Mungu na ikakuinua na kukufariji sana. Tunaendelea kuishi na kufanya kazi, sio kwa sababu ya mastahili yetu, bali kwa sababu tu ya Huruma ya Mungu. Tunataka sasa kuienzi huruma hiyo ya Mungu kwa kuielekeza kwa binadamu wenzetu. Tuishi katika huruma ya Mungu, hata tufapo, tufe katika Huruma ya Mungu. Tusikilizane kipindi kijacho wakati kama huu.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB








All the contents on this site are copyrighted ©.