2015-04-20 08:13:00

Hija ya kitume Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon: fursa na changamoto


Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon, kuanzia tarehe 20 Aprili 2015 linaanza kufanya hija ya kitume mjini Vatican inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano. Ni nafasi ya kukutana, kusali na kushirikishana maisha na utume wa Kanisa mahalia na Baba Mtakatifu pamoja na waandamizi wake. Ni wakati pia wa kuimarishana katika imani, matumaini na mapendo, kwa kuonesha umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon, linafanya hija hii likiwa linakabiliana na changamoto za ujenzi wa misingi ya haki, amani na umoja wa kitaifa; imani za kishirikina zinazotishia Injili ya Uhai; ujenzi na ukuzaji wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, dhidi ya vitisho vya Injili ya Familia. Kanisa linaendelea kuwa ni mdau mkuu katika sekta ya elimu, afya na maendeleo jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon linabainisha kwamba, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza, kama sehemu ya mchakato wa kupambana na ujinga, maradhi na umaskini wa hali na kipato. Tangu mwaka 2009 kulipotokea machafuko ya kisiasa kutokana na uchaguzi mkuu uliofanyika wakati huo, Maaskofu wamekuwa wakiitaka Serikali kuhakikisha kwamba inafanya chaguzi zinazojikita katika misingi ya ukweli, uwazi na demokrasia kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Kanisa linahamasisha utamaduni wa kutafuta na kudumisha mafao ya wengi kwa kuzingaria matumizi sahihi ya rasilimali na utajiri wa nchi na kwamba, Kanisa litaendelea kuwa ni Sakramenti ya haki, amani na upatanisho; changamoto ya kuendeleza majiundo makini kwa Familia ya Mungu nchini Gabon, ili iweze kutekeleza dhamana hii kwa ufanisi mkubwa.

Maaskofu Katoliki Gabon wanasema kwamba, imani za kishirikina zinahatarisha Injili ya Uhai, utu na heshima ya binadamu. Ndiyo maana kunako mwaka 2012, Kanisa Katoliki nchini Gabon likaanzisha Siku ya Kitaifa kwa ajili ya kuombea waathirika wa imani za kishirikina; tukio ambalo liliwashirikisha hata waamini wa madhehebu na dini mbali mbali nchini humo pamoja na Serikali kuangalia upya sheria za nchi kuhusiana na vitendo vinavyosababaisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kutokana na imani za kishirikina.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon linafafanua kwamba, linaendeleza majadiliano ya kiekumene na waamini wa madhehebu mbali mbali ya Kikristo katika misingi ya ukweli katika upendo na umoja katika Kristo; ili Wakristo wote waweze kuwa kweli ni mashuhuda wenye mvuto na mguso katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa nchini Gabon linasema kwamba, litaendelea kusimama kidete kulinda, kutetea, kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia kwa kukazia tunu bora za maisha ya ndoa na familia mintarafu Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa. Kanisa linapinga utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba, kifo laini na ndoa za watu wa jinsia moja. Ikumbukwe kwamba, familia inajengwa kutokana na upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo.

Kanisa Katoliki nchini Gabon, ni mdau mkubwa katika utoaji wa huduma makini kwenye sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Mwaka 2015, Jimbo kuu la Libreville, limeadhimisha Jubilee ya miaka 170 tangu shule ya kwanza ya msingi ilipofunguliwa nchini humo. Kanisa linachangia kwa kiasi kikubwa katika majiundo makini ya wananchi wa Gabon, kiroho na kimwili. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon kwamba, Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Kanisa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii ili kuweza kutoa huduma makini kwa Familia ya Mungu nchini Gabon.

Baraza la Maaskofu Katoliki Gabon linasema, sekta ya mawasiliano ya jamii bado ni changamoto kubwa inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuliwezesha Kanisa kuendeleza dhamana na utume wake kama sauti ya kinabii. Baraza la Maaskofu lina miliki na kuendesha kituo kimoja cha Radio pamoja na Gazeti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.