2015-04-20 07:53:00

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa: maridhiano na upatanisho!


Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha kitume cha Wafokolari kwa mwaliko wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon anatarajiwa kushiriki katika Baraza kuu la Umoja wa Mataifa linalojadili kuhusu “Uhamasishaji wa maridhiano na upatanisho; ili kudumisha jamii katika misingi ya amani na ukarimu dhidi ya misimamo mikali ya kiimani”. Mkutano huu unahudhuriwa na wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa na kwamba, kuna viongozi kadhaa wa kidini wamealikwa kushiriki.

Baraza la kuu la Umoja wa Mataifa linafanya kikao hiki kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Aprili 2015 na kwamba, siku ya kwanza ya kazi, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa watapembua kwa kina mapana kuhusu mada hizi na siku ya pili, viongozi wa kidini watashirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano; kwa kuzingatia uhudu wa kuabudu na haki msingi za binadamu sanjari na kujikita katika kutafuta na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Lengo na mkutano huu ni kuiwezesha Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kujenga na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini, ambayo imekuwa ni chanzo cha maafa mengi ya watu wasiokuwa na hatia na kikwazo cha ustawi na maendeleo ya wengi. Kadiri ya ajenda za Umoja wa Mataifa baada ya mwaka 2015, Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zinatakiwa kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa ujenzi wa maridhiano na upatanisho kati ya watu; mambo msingi katika kudumisha amani ya kweli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.