Vatican inaendelea na maombolezo ya kuondokewa na watumishi wake katika Dekania ya Makardinali, kufutia kifo kingine kilichotokea Ijumaa usiku tarehe 17 April 2015, cha Kardinali Francis E. George, OMI, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Chicago, Marekani. Marehemu aliyestaafu mwaka jana 2014, pia aliwahi kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani (USCCB) kati ya mwaka 2007-2010. Kardinali George, amefariki akiwa na umri wa miaka 78, baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kansa kwa muda mrefu .
Baba Mtakatifu Francisko, baada ya kupoeka taarifa hizi, amepeleka salaam zake za rambi rambi kwa njia ya telegram iliyotiwa sahihi na Katibu wa Jimbo la Papa,Kardinali Pietro Parolin, kwa Askofu Mkuu Blase Cupich wa Jimbo Kuu la Chicago, ambamo ameonyesha kusitikishwa na taarifa hizo . Papa ametoa rambirambi hizi kwa Mapadre , watawa na waamini wote wa Jimbo Kuu la Chicago, na pia kwa mwakilishi wake nchi Marekani,Askofu Mkuu Carlo Maria Viganò.
Papa ameyakumbuka maisha na utumishi wa Marehemu
na kutoa shukrani kwa ushuhuda ulioonyeshwa na Kardinali George katika maisha ya
kujitenga kama mwanashirika wa Oblate ya Mary Immaculate, na kwa utumishi wake
katika utume wa elimu, na huduma yake ya kiaskofu katika Makanisa ya Yakima, Portland
na Chicago. Kwa moyo wa majonzi, amesema, anaungana na wote katika sala za kuiombea
roho ya Mtumishi huyo aliyekuwa amejaliwa hekima,busara na unyenyekevu wa kichungaji,
kupokelewa katika upendo na huruma ya Mungu Baba yetu wa mbinguni. Aidha Papa amefariji
wote wanaoombeleza msiba huu, na tumaini la uhakika la ufufuo, na kuwaomba wapokee
Baraka zake za upendo wa Kitume kama amana ya faraja na amani katika Bwana.
Askofu Mkuu Kurtz wa Jimbo la Luisville Kentucky , ambaye pia ni Rais wa USCCB, akitangaza kifo cha Kardinali George, anasema , kifo cha mtumishi huyu wa kanisa, kinatia simanzi zaidi, hasa wakati huu wa furaha ya ufufuko wa Bwana. Na kwamba alikuwa ni mtumishi mwema wa kanisa, mfano wa kuigwa na wengi . Na pamoja na kuhuzunika lakini pia wanapata kuwa na amani ya moyo katika utambuzi kwamba, baada ya mateso mengi, sasa ameikamilisha safari yake katika mkono wa Bwana . Uongozi wake hautasahaulika akiwa Askofu Mkuu wa Chicago na Rais wa USCCB, ambamo aliwaongoza kwa ukarimu na unyenyekevu mkubwa , akihimiza kila mmoja kuona jinsi Mungu ambavyo hutufanya wote kuwa familia moja, kaka na dada, mmoja na mwingine.
Askofu Kurtz, akiwa ameungana na ndugu zake katika uaskofu, kumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi ya maisha ya ushuhuda ya Kardinali George, na amewaalika waamini wote kumkumbuka katika sala zao, kuombea nafsi yake ipate pumziko la amani.
All the contents on this site are copyrighted ©. |