2015-04-18 08:57:00

Sinodi ya Familia: Simameni kidete kutangaza Injili ya Familia


Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon katika mkutano wake wa 40 wa mwaka uliokuwa unafanyika mjini Yaoundè, umetoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu mazingira na tamaduni bora nchini Cameroon. Mada hii ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba, 2015 mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon linabainisha kwamba, lengo si kutangaza wala kufafanua mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusiana na maisha ya ndoa na familia, bali ni kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia katika uhalisia wa maisha ya wananchi wa Cameroon. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maisha ya ndoa na familia, kiasi hata cha kutishia kutikisa misingi  ya maisha ya ndoa na familia. Kanisa linapenda kuwajengea waamini uwezo ili kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika mwanga wa Injili, ili ziweze kutekeleza dhamana na wito wake katika maisha na utume wa Kanisa.

Askofu mkuu Samuel Klèda, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Cameroon anasema kwamba, ustawi na maendeleo ya nchi yanategemea sana jinsi ambavyo nchi inawezeka katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kumbe, Kanisa halina budi kuisaidia Serikali katika mchakato wa kuboresha sera na mikakati ya maisha ya ndoa na familia anasema Bibi Marie-Therese Abèna Ondoa, Waziri wa wanawake na familianchini Cameroon. Kanisa lina mchango mkubwa katika sekta ya elimu pamoja na kuwafunda wananchi katika medani mbali mbali za maisha na kwamba, Taasisi hizi mbili ingawa zina majukumu tofauti, lakini zinakamilishana katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Jean Mbarga wa Jimbo kuu la Yaoundè anabainisha umuhimu wa maisha ya ndoa na familia kwani hiki ni kiini cha jamii, kumbe kuna haja ya kuzisaidia familia ili ziweze kutekeleza dhamana na wito wake kikamilifu. Familia inaundwa katika mshikamano wa upendo wa dhati kati ya Bwana na Bibi na wala si vinginevyo. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai na Utakatifu wa maisha, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha ya watu.

Ili kulinda na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kupambana na hatimaye, kukomesha kabisa mashambulizi yanayofanywa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, ambacho kwa sasa kimekuwa ni chanzo cha maafa makubwa kwa wananchi wengi ndani na nje ya Nigeria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.