2015-04-17 08:38:00

Simameni kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai na Familia!


Maaskofu Katoliki kutoka Jimbo kuu la Ibadan, Nigeria, katika mkutano wao wa kimataifa uliohitimishwa hivi karibuni, wamekazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kusimama kidete kulinda na kutangaza Injili ya Familia inayojikita katika upendo thabiti kati ya Bwana na Bibi, kadiri ya mpango wa Mungu kwa binadamu na kwamba, matunda ya muungano huu ni watoto ambao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maaskofu wanapenda kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika kukuza na kudumisha mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume kwa familia, ili ziweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara. Mkutano wa Maaskofu hawa ulikuwa unaongozwa na kauli mbiu “kulinda maisha ya binadamu na tunu msingi za familia dhidi ya utamaduni wa kifo”.

Maaskofu wakizungumza na waandishi wa habari wanabainisha kwamba, familia katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia inakumbana na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali, ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko kwa busara na hekima ya kichungaji, aliamua kuitisha Sinodi mbili kuhusu familia kwa ajili ya kupembua kwa kina na mapana changamoto hizi, ili kuliwezesha Kanisa kuwa na mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya maisha na utume wa familia. Lengo ni kuwawezesha wanandoa kuendelea kutangaza kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu Injili ya Familia.

Maaskofu wamepambanua sera na mikakati inayoweza kutumiwa na Mama Kanisa ili kusimama kidete kulinda na kutetea utakatifu, utu na heshima na dhamana ya familia ya binadamu, dhidi ya utamaduni wa kifo unaoendelea kukumbatiwa na baadhi ya watu kwa njia ya vitendo vya kigaidi, mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa imani za kishirikina; utekaji nyara, ujambazi, ajali barabarani pamoja na baadhi ya watu kukata tamaa na hatimaye, kutema zawadi ya uhai kwa kujinyonga. Kutokana na matukio yote haya, Kanisa linaona kwamba, ni wajibu na dhamana yake, kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai, ili kuwasaidia waamini kutambua utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Maaskofu wanawaalika wanandoa kuwapokea watoto wanaozaliwa katika familia zao kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili kuendelea kuenzi Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Watu waepuke kishawishi cha kutaka kukumbatia utamaduni wa kifo kwa kujikita katika sera za utoaji mimba. Waheshimu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kamwe wasikubali kukengeuka kwa kutafuta uhuru usiokuwa na mipaka wala maadili kwa kisingizio cha mtu kujiamria mambo yake mwenyewe, hata kama yanasigana na kanuni maadili na utu wema.

Maaskofu wanasema mielekeo na ndoa za watu wa jinsia moja ni tatizo kubwa katika maisha ya ndoa na familia na kwamba, wasingependa kuona mmong’onyoko huu wa kimaadili na utu wema, unapigiwa “debe” ili kuhalalishwa kisheria. Haki ya uzazi salama kwa wanawake ni dhana inayokumbatia pia utamaduni wa kifo. Wananchi wa Nigeria wasikubali hata kidogo kutumbukizwa katika ombwe la watu kukengeuka kimaadili kwa madai ya uhuru wa mtu!

Maaskofu wanasema kwamba, maisha ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amemkirimia mwanadamu na kamwe haiwezi kugeuzwa kuwa ni bidhaa inayoweza kuuzwa au kununuliwa dukani. Uzazi kwa njia ya chupa ni kutaka kumweka Mwenyezi Mungu majaribuni na kwamba, biashara haramu ya binadamu na viungo vyake ni uhalifu dhidi ya binadamu. Umefika wakati kwa Serikali kushirikiana na wadau mbali mbali ili kusimamia kikamilifu utu wa binadamu, maisha na haki zake msingi. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wasimame kidete kutangaza Injili ya Uhai na kukata katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo. Wawe ni mfano bora wa Injili ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.