2015-04-15 15:39:00

P. Lombardi: Kanisa limempoteza kiongozi wa shoka!


Kardinali Roberto Tucci, mtawa Myesuiti amefariki dunia wakati Mama Kanisa anaadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani, mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wake, kwa kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Ni mtawa aliyezamisha maisha yake katika sala, adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na maisha ya kijumuiya, mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Mama Kanisa katika maisha na utume wa watawa!

Kardinali Tucci alitambua dhamana na utume wake ndani ya Kanisa, akawa tayari kutekeleza kazi mbali mbali alizodhaminishwa na Mama Kanisa. Akiwa bado mtawa kijana, aliteuliwa kuwa ni Mkurugenzi wa Jarida maarufu linalochapishwa na Wayesuit, yaani “ La Civiltà Cattolica”. Aliteuliwa kushiriki katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama mtaalam na akasaidia sana kuhariri Waraka wa Kanisa Ulimwenguni, “Gaudium et spes”.

Kardinali Tucci alishiriki kikamilifu katika mchakato wa mawasiliano wakati wa maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwamba, waandishi wengi wa habari waliofuatilia maadhimisho ya Mtaguo mkuu wa Pili wa Vatican wanamkumbuka kwa umakini na umahiri wake katika kufafanua, kupembua na kuchambua maisha na utume wa Kanisa. Kama  mkurugenzi mkuu wa Jarida la Civiltà Cattolica, alikuwa na uwezo mkubwa wa kugawa majukumu kwa wasaidizi wake wote, wakajiamini na kutekeleza dhamana yao bila wasi wasi.

Huu ni ushuhuda unaotolewa na Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican na mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican ambaye alibahatika kufanya kazi kwa karibu sana na Kardinali Roberto Tucci. Kama mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican kazi yake ilikuwa finyu kidogo, kwani alikabidhiwa dhamana ya kuratibu na kusimamia hija za kitume za Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, lakini hata bila uwepo wake, aliweza kutoa ushauri ambao ulifanyiwa kazi na Radio Vatican ikasonga mbele.

Kardinali Tucci ni mtawa aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika maisha na utume wake, akajipambanua kuwa mratibu mahiri sana katika kupanga na kutekeleza hija za kitume zilizofanywa na Papa Yohane Paulo II sehemu mbali mbali za dunia. Aliweza kupanga na kuamua mambo makuu katika hali ya unyenyekevu, busara na akili. Alijenga mahusiano mema na wawakilishi wa Vatican na wakuu wa serikali na nchi mbali mbali kiasi kwamba, hija za kitume zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II zimebaki kuwa gumzo katika mataifa mbali mbali.

Mtakatifu Yohane Paulo II akatambua ushupavu wa Padre Roberto Tucci katika maisha na utume wake kama mtawa, akamteuwa kuwa Kardinali kama kielelezo cha huduma iliyotukuka ndani ya Kanisa na mfano wa kuigwa pasi na makuu. Ni kiongozi aliyejisadaka na kuacha yote kwa ajili ya kuratibu hija za Khalifa wa Mtakatifu Petro, huduma nyeti sana katika maisha na utume wa Kanisa anasema Padre Federico Lombardi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.