2015-04-15 12:38:00

Kardinali Roberto Tucci amefariki dunia


Tunasikitika kutangaza kifo cha  Kardinali Roberto Tucci, kilichotokea siku ya Jumanne  usiku mjini  Roma, ikiwa zimebaki siku chache kutimiza miaka 94 ya kuzaliwa hapo tarehe  19 Aprili. Kardinali Tucci alijiunga na Wajesuit na kupata daraja la Upadre mwaka  1950, na baadaye alijipatia shahada ya uzamili  katika masomo ya kitaalimungu  katika Chuo Kikuu cha Kipapa Gregorian kilichoko mjini Roma


Pamoja na huduma za kikuhani, pia alifundisha kwa miaka kadhaa katika Kitivo Teolojia katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu  Louis  cha Naples,  pia akiwa Mkurugenzi wa jarida la Wajesuit la Civilta Catolica kati ya mwaka 1959-1973. Na baadaye akateuliwa  kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Redio Vatican, utume alioutumikia   kati ya 1973-1985. Alifanywa Kardinali na Papa Yohana Paul II  mnamo Februari 21, 2001. Kati ya majukumu mengine , aliwahi pia kuwa mratibu wa safari za  Papa Yohana Paul II. .

Aidha Marehemu Kardinali Tucci, anakumbukwa kwa kazi kubwa aliyoifanya wakati wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Vatican ,ambamo alishiriki kazi za  kuandaa  nyaraka za majadiliano ya Baraza,  na  vikao mbalimbali kama mtalaam wa teolojia.  Pia alitoa mchango mkubwa  katika  toleo la mwisho la Katiba ya Kichungaji “Gaudium et Spes”

Taarifa imetolewa kwamba, Jumatano 15 Aprili, majira ya saa sita, katika Jengo la Makao Makuu ya Wajesuit hapa Roma, Mtaa wa Borgo San  Spirito Namba 4, Mwili wa Marehemu utaweka katika  chumba maalu , kwa ajili ya  kutoa heshima za Mwisho  kwa Marehemu. Siku ya Ijumaa 17 Aprili majira ya saa saba na nusu za mchana , Mwili wa Marehemu  utahamia katika Altare ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, kwa ajili ya Ibada ya Misa ya wafu na Maziko, itakayoongozwa na Kardinali Angelo Sodano , Mkuu wa Dekania ya Makardinali, majira ya saa kumi na nusu za jioni. Papa Francisko , ataongoza Ibada ya mazishi.  Tunaiombea Roho yake pumziko la amani. 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.