2015-04-15 09:35:00

Expo 2015 na mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani


Kardinali Gianfranco Ravasi,  Rais wa Baraza la Kipapa la utamaduni anabainisha kwamba, Vatican inashiriki katika Onesho la Chakula Kimataifa mjini Milano, Expo 2015 kwa kuonesha mambo msingi katika banda yake. Lengo si kuonesha bidhaa za mazao ya kilimo bali ni kutoa ujumbe unaoichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kwa ajili ya kumhudumia mwanadamu katika mahitaji yake msingi. Onesho la Expo 2015 linazinduliwa rasmi tarehe Mosi, Mei hadi na kuendelea hadi tarehe 31 Oktoba 2015.

Banda la Vatican anasema, Kardinali Ravasi linataka kuonesha changamoto kubwa na endelevu inayojikita katika kauli mbiu “Si mkate peke yake” na “Utupe leo chakula chetu”. Ni vifungu vya maneno kutoka katika Maandiko Matakatifu vinavyoichangamotisha Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inazalisha chakula bora na cha kutosha kwa ajili ya kukidhi mahitaji msingi ya binadamu; umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya mafao ya wengi na kwamba watu wanapaswa kujifunza utamaduni wa kushirikishana chakula na jirani zao.

Si haki kwamba, kuwa watu wanakula na kusaza, wakati ambapo kuna mamillioni ya watu wanakufa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Vatican katika onesho hili inataka kukazia utandawazi unaojikita katika umoja na mshikamano wa kidugu. Ni onesho linalopania kuelimisha kwamba, mkate unaomegwa ni kielelezo cha Ekaristi Takatifu, uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake. Onesho la chakula kimataifa lina uhusiano wa pekee na maisha ya kiroho na kwa namna ya pekee na Ekaristi Takatifu, chakula cha maisha ya kiroho, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Banda la maonesho la Vatican linasimamiwa na Baraza la Kipapa la utamaduni kwa kushirikiana na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI pamoja na Jimbo kuu la Milano, ambalo ni mwenyeji wa Onesho la Expo 2015. Monsinyo Domenico Pompili, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anabainisha kwamba, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na changamoto za uhaba wa chakula na lishe duni. Hii ni changamoto kubwa kwani twakimu zinaonesha kwamba, kuna zaidi ya watu millioni nne wanaokabiliwa baa la njaa duniani.

Kanisa linapenda kuihamaisha Jumuiya ya Kimataifa kushikamana kwa dhati ili kupambana na baa la njaa duniani, kashfa ya karne ya ishirini na moja. Dini mbali mbali zinahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani.

Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, “Cor Unum” ambalo linaendelea kuhamasisha mshikamano katika mapambano ya baa la njaa duniani, ili kulinda, kujenga na kuendeleza amani na utulivu, linafafanua kwa kina mapana kuhusu ujumbe wa Neno la Mungu mintarafu mahitaji msingi ya binadamu. Cor Unum imeandaa picha mbali mbali zinazonesha madhara ya baa la njaa na utapiamlo sehemu mbali mbali za dunia pamoja na huduma makini inayotolewa na Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki, Caritas huko Burkina Faso, Ecuador na Iraq. Hapa mkazo unawekwa kwenye mshikamano wa upendo unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa. Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Hospitali ya Bambino Gesù wanashiriki.

Kwa wale wanaotaka kufahamu zaidi kuhusu ushiriki wa Vatican katika onesho la Expo 2015 wanaweza kutembelea tovuti maalum ya tukio hili kwa anuani ifuatayo:

www.expoholysee.org

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.