2015-04-15 08:16:00

Boko Haram ishikishwe adabu; mateka warejeshwe kwenye familia zao!


Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, utekaji nyara wa wasichana wa shule ya Chibok, Nigeria ni pigo kubwa sana kwa familia na jamii ya Nigeria katika ujumla wake, lakini hadi wakati huu, Kanisa linapenda kuwahakikishia wazazi wa wasichana waliotekwa nyara kwamba, liko pamoja nao katika shida na mahangaiko yao.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaonesha wasi wasi mkubwa ikiwa kama kweli wasichana hao bado wangali hai au tayari wamekwishafariki dunia au kugeuzwa kuwa ni wanawake wa wanajeshi wa kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, jambo ambalo linadhalilisha utu na heshima ya wasichana hawa. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria linaendelea kuwashukuru wadau mbali mbali ambao wameongeza nguvu katika mapambano dhidi ya kikundi cha Boko Haram ambacho kwa mwaka mmoja, kimekuwa ni chanzo cha mauaji ya kutisha na uharibifu mkubwa wa mali za watu na miundo mbinu ya huduma mbali mbali za kijamii na kiuchumi.

Changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, Boko Haram inadhibitiwa na wasichana waliotekwa wanapatikana na kurejeshwa tena kwenye familia zao, jambo ambalo Serikali ya Nigeria inasema kwamba, ni vigumu, lakini Rais mteule Muhammadu Buhari anasema, Serikali yake itajitahidi kufanya kinachowezekana, kwani kama mwanajeshi mstaafu anafahamu fika mapungufu ya kijeshi na intelijensia ya nchi; mambo ambayo hana budi kuyavalia njuga, ili kweli: haki, amani, utulivu na ustawi wa wengi vianze kurejea tena nchini Nigeria, ambako kwa sasa watu wanaishi kwa wasi wasi na woga mkuu. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwamba, Serikali mpya, itaweza kubainisha mbinu mkakati wa kukishinda kikundi cha Boko Haram na watu waliotekwa nyara kuweza kurejeshwa tena makwao. Boko Haram bado inaendelea hadi sasa kufanya mashambulizi ya kushtukiza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.