2015-04-14 14:14:00

Ratiba elekezi ya hija ya Papa Francisko nchini Bosnia na Erzegovina


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Bosnia na Erzegovina, hapo tarehe 6 Juni 2015, ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani na kujikita katika majadiliano ya kidini, ili kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Ratiba iliyotolewa na Vatican inaonesha kwamba:

Saa 9: 00 majira ya asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko atapokelewa rasmi kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Sarayevo na baadaye atamtembelea Rais wa Watu wa Bosnia na Erzegovina, Ikulu ambayo iko karibu na Uwanja wa ndege.

Saa 4: 10 asubuhi, Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na viongozi wa serikali na wanadiplomasia nchini humo. Na saa 5:00 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kosevo na baadaya atapata nafasi ya kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Bosnia na Erzegovina pamoja na kupata nao chakula cha mchana, kwenye Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini humo.

Saa 10: 20 jioni, Baba Mtakatifu atakutana na Mapadre, watawa, waseminari kwenye Kanisa kuu na hapo atazungumza nao. Majira ya saa 11: 30 jioni, Baba Mtakatifu atakutana na viongozi wa dini mbali mbali nchini humo katika Kituo cha Wafranciskani kwa ajili ya wanafunzi kimataifa.

Saa 12: 30 jioni, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na kuzungumza na vijana kwenye kituo cha Vijana cha Yohane Paulo II na baadaye, ataelekea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Sarayevo, tayari kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake.Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kukujuza yale yanayojiri katika hija hii ya kitume. Lakini kwa wale wenye haraka zao, wanaweza kila wakati kutembelea mtandao wa Radio Vatican kwa habari zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.