2015-04-14 10:14:00

Mwaka Mtakatifu: kiwe ni kipindi cha kujenga umoja na mafao ya wengi


Mwaka wa Mtakatifu wa Huruma ya Mungu uliotangazwa rasmi na Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu, tarehe 11 Aprili 2015 ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, ni muda uliokubalika wa kukimbilia msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, ni muda wa mshikamano wa upendo na udugu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Misericordiae vultus” “Uso wa huruma” anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali katika misingi ya ukweli, uwazi na kukataa katu katu kishawishi cha kutumia mabavu na ubaguzi kwa misingi ya kidini. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa huruma ya Mungu, iwe ni nafasi makini ya kuchuchumilia umoja, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa; ili kwa pamoja watu waweze kutangaza huruma ya Mungu inayogusa undani wa maisha yao ya kila siku.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu ambaye pia ni Rais wa Mashirika ya kimissionari ya kipapa anasema, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema wakati huu kwa namna ya pekee, anapenda kuyaelekeza mawazo na nia yake nchini Tanzania, ili kweli maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu uweze kuleta umoja na maridhiano nchini Tanzania kwa kuanzia katika familia, jamii na taifa katika ujumla wake.

Jubilee ya huruma ya Mungu kiwe ni kipindi cha kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya watanzania wote, ili hatimaye, kujenga jamii inayojipambanua katika misingi ya: haki, amani, furaha na ustawi sanjari na mshikamano wa kitaifa; mambo ambayo kwa miaka mingi yamekuwa ni utambulisho wa watanzania. Lakini kwa sasa hali si shwari sana, kuna mpasuko unaopaswa kushughulikiwa haraka iwezekanvyo kwa kujikita katika huruma, hekima na busara ya Kimungu.

Tanzania inakabiliwa na mchakato wa kura ya maoni kwa ajili ya Katiba inayopendekezwa, zoezi ambalo limewagawa watanzania kwa misingi ya kisiasa na kidini. Watanzania wanajiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani; huu nao ni moto wa kuotea mbali; ni mambo nyeti na tete kwa usalama, maisha na ustawi wa watanzania wengi.

Askofu mkuu Rugambwa anawataka watanzania wote kushikamana katika umoja na maridhiano ya kitaifa, ili pale ambapo kumekuwepo na hali ya kutoelewana, kuvutana na kinzani, watu wawe na ujasiri wa kuyaweka kando na kuanza mchakato kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi. Ni mwaliko wa kuyaweka matukio yote haya mbele ya huruma, hekima na busara ya Kimungu, kwa ajili ya sifa na utukufu wa Mungu na maendeleo ya watanzania wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.