2015-04-13 09:43:00

Mapambano dhidi ya baa la umaskini ni dhamana ya kimaadili na kiroho


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inatokomeza umaskini wa hali na kipato ifikapo mwaka 2030, kwani hii ni dhamana ya kimaadili na maisha ya kiroho. Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Mashirika ya misaada ya Makanisa kimataifa, ikiwemo Caritas Internationalis na Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Hii ni changamoto na mbinu mkakati unaofanyiwa kazi na Shirikisho la Mabenki Duniani, ambalo hivi karibuni limekutana na kuzungumza na viongozi wa mashirika ya misaada ya Makanisa mbali mbali duniani. Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya watu billioni moja ambao wanaendelea kukandamizwa na baa la umaskini wa hali na kipato sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kudhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Katika tamko lao, mashirika ya misaada ya Makanisa yanasema kwamba, kama makundi yanayowakilisha masuala ya kiimani wanayo dhamana ya kimaadili na maisha ya kiroho kuwasaidia watu kujifunga kibwebwe kupambana na baa la umaskini wa hali na kipato, ili kuboresha maisha yao. Umaskini wa hali na kipato ni changamoto kubwa kwa dini na serikali mbali mbali duniani, kumbe kwa pamoja wanaweza kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.