2015-04-12 09:35:00

"Vita ni upuuzi na majanga ya mwanadamu kujitakia mwenyewe"


Ulimwengu mamboleo umesheheni wasi wasi na hofu kubwa kutokana na majanga yanayoendelea kujitokeza katika maisha ya mwanadamu kiasi kwamba, watu wengi wanajiona kuwa dunia iko katika mapambano ya vita kuu ya tatu ya dunia. Kuna Wakristo wengi wanaoendelea kuteseka na kuuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Hata leo hii bado kuna watu ambao hawaguswi hata kidogo na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Wananchi wa Armenia hata wao pia wamekumbana na mauaji ya kimbari yaliyotokea miaka mia moja iliyopita; hapa viongozi wa Kanisa na waamini wengi waliuwawa kikatili. Bado watu wengi wanaukumbuka ukatili wa vita kuu ya kwanza na ya pili ya dunia bila kusahau mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Cambodia, Rwanda, Burundi na Bosnia. Familia ya binadamu kamwe haijafaulu kujifunza kutokana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, kwani hata leo hii bado kuna watu wanaoendeleza mauaji ya kikatili na watu wengine wakiendelea kuwa ni watazamaji tu. Bado binadamu hajajifunza kwamba,  vita ni upuuzi na majanga ya kujikitakia.

Hizi ni salam za Baba Mtakatifu Francisko kwa Familia ya Mungu kutoka Armenia alizozitoa Jumapili tarehe 12 Aprili 2015 kabla ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbu kumbu ya miaka mia moja tangu mauaji ya kimbari yalipotokea nchini Armenia na kusababisha majanga makubwa. Ibada hii imehudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali na wa Kanisa kutoka Armenia. Hii ni kumbu kumbu inayogusa mioyo ya watu iliyojeruhiwa, lakini yenye matumaini katika ufufuko wa Yesu Kristo. Kumbu kumbu hii ni muhimu ili kuponya majeraha ya madonda ya mauaji ya kimbari.

Baba Mtakatifu anasema waamini wanafundishwa kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwema na mwingi wa huruma na mapendo, kamwe hawezi kuwa ni sababu ya ukatili au kuhalalisha mauaji kwa jina lake. Maadhimisho haya yanafanyika wakati waamini wakiwa wanayaelekeza macho yao kwa Kristo Mfufuka, aliyeshinda dhambi na mauti.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.