2015-04-11 16:51:00

Kanisa ni alama: chombo cha huruma ya Mungu, iweni mashuhuda wa huruma


Amani iwe kwenu ni salam inayoendelea kusikika ingawa bado kuna watu wanaoendelea kukabiliana na vita, nyanyaso na dhuluma katika maisha yao, kwa vile tu ni Wakristo. Mama Kanisa anaendelea kupaaza sauti ya kilio chake kwa Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, ili aweze kuimarisha imani ya Wakristo wanaoteseka pamoja na kuendelea kuomba ili watu watubu na kumwongokea Mungu kwa kuguswa na mteso pamoja na mahangaiko ya watu hao.

Binadamu amekombolewa kwa njia ya Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Yesu Kristo na kwamba, yeye ni kielelezo cha upatanisho anayeishi kati ya watu wake, ili kuwaonesha njia ya upatanisho kati ya Mungu na jirani zao. Licha ya magumu na suluba za maisha, lakini bado waamini wana matumaini ya wokovu ambao upendo wa Yesu Kristo umepandikiza katika mioyo ya watu. Huruma ya Mungu imemiminwa mioyoni mwa waamini kiasi cha kuwafanya kuwa wenye haki na kuwakirimia amani.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa masifu ya Jumapili ya kwanza ya huruma ya Mungu, tarehe 11 Aprili 2015, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kanisa linapenda kuadhimisha Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu kwa kuonesha uwepo wa Mungu kati ya watu wake, nyakati hizi ambazo kuna mabadiliko makubwa, ili kuangalia mambo msingi katika maisha. Ni kipindi kwa Mama Kanisa kuangalia maisha na utume wake, ili kuwa ni alama na chombo cha huruma ya Mungu.

Jubilee ya mwaka wa huruma ya Mungu, iwe ni fursa kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba anaona na kutambua wema na huruma ya Mungu inayotolewa ulimwenguni, hususan kwa wanaoteseka, wapweke na waliotelekezwa na wakati mwingine pasi ya kujisikia kwamba, wanapendwa na wamesamehewa na Mwenyezi Mungu. Ni mwaka mtakatifu unaowataka Wakristo kujisikia furaha ya kuweza kukutana na Yesu, kama ilivyo kwa mchungaji mwema, anawabeba mabegani mwake, ili kuwarejesha tena nyumbani mwa Baba yake wa mbinguni.

Mwaka huu mtakatifu, uwajalie waamini kuguswa na Yesu ili waweze kugeuzwa kwa njia ya huruma yake, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu. Hizi ndizo sababu msingi anasema Baba Mtakatifu zilizomsukuma kutangaza Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, kwani hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu. Huu ni muda uliokubalika wa kuganga na kutibu madonda, bila ya kuchoka kukutana na watu ambao wana matumaini ya kuona na kuguswa na alama ya uwepo wa karibu wa Mungu katika maisha yao, ili kuwakirimia wote msamaha na upatanisho. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu asaidie kufungua macho ili kuona dhamana ambayo wanaitiwa, awaombee waamini neema ya kuweza kuishi kikamilifu maadhimisho ya Mwaka wa Jubilee ya huruma ya Mungu, kwa njia ya ushuhuda aminifu na tendaji.

Wakati wa masifu ya jioni, Baba Mtakatifu Francisko amewapatia wawakilishi wa Makanisa makuu ya Kipapa ya Jimbo kuu la Roma na wawakilishi wa Mabara nakala ya Waraka wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu ujulikanayo kama “Misercordiae vultus” ”Sura ya huruma” utakayosomwa pia kwa Makanisa mahalia kadiri ya maelekezo yaliyomo kwenye Waraka huu wa kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.