2015-04-11 15:40:00

Jengeni utandawazi wa mshikamano, umoja na udugu!


Majadiliano ya kina na ushirikiano thabiti ni mambo msingi katika kukoleza na kudumisha mshikamano wa pamoja, kwa ajili ya mafao ya wengi sanjari na kuondokana na mambo ambayo yanawagawa wananchi wa Bara la Amerika. Kwa watu kushirikiana katika tunu msingi za maisha ya kijamii, wanaweza kufikia mchakato unaowawezesha kufungamana kitaifa, kikanda na kimataifa, kwa kupambana na matatizo, ili hatimaye, kuwaonjesha raia wao matumaini mapya.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliomwandikia Rais Juan Carlos Varela Rodrigues wa Panama na kusomwa na Kardinali Pietro Parolin wakati wa mkutano wa wakuu wa nchi Barani Amerika uliofanyika nchini Panama, kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Ustawi katika usawa: changamoto katika ushirikiano Barani Amerika”.

Baba Mtakatifu anaunga mkono kauli mbiu hii na kuendelea kukazia dhamana ya usawa na haki katika ugawaji na matumizi ya utajiri na rasilimali ya nchi mambo ambayo wakati mwingine yamekuwa ni chanzo cha kinzani na migogoro ya kijamii. Utajiri na rasilimali ya nchi haina budi kutumiwa kikamilifu kwa ajili ya kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kwa kusaidia maboresho ya mahitaji msingi ya binadamu kama vile: kazi na makazi; huduma za kijamii: elimu na afya; usalama na utunzaji bora wa mazingira; mambo ambayo kila binadamu anapaswa kuhusishwa kikamilifu bila kutengwa hata kidogo.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, ukweli wa mambo unaonesha kwamba, bado kuna watu wengi wanakabiliana na ukosefu mkubwa wa usawa, kinyume cha haki na kwamba, changamoto kubwa kwa ulimwengu mamboleo ni utandawazi wa mshikamano; udugu; kinyume cha utandawazi usiojali na unaojikita katika ubaguzi; hali inayopelekea kutokuwepo kwa mgawanyo sawa wa raslimali na hivyo kinzani na migogoro ya kijamii kuendelea kushamiri kwa kasi kubwa.

Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, mataifa mengi anasema Baba Mtakatifu yamecharuka katika mikakati ya maendeleo endelevu, lakini pia kuna nchi ambazo zimebaki nyuma kimaendeleo na hivyo dunia kuendelea kugawanyika kati ya nchi maskini na tajiri; maskini kuendelea kuogelea katika shida na mahangaiko mbali mbali, wakati matajiri wakiendelea kufaidika na utajiri wa dunia. Kanisa kwa upande wake, linapenda kukazia maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anapenda kukazia kuhusu tatizo na changamoto ya wahamiaji kwa kuangalia kwa kina na mapana mambo ambayo yanapelekea baadhi ya wananchi kuamua kuzikimbia nchi zao, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao ka kujikuta wanatumbukia katika wafanyabiashara haramu wa binadamu, utumwa mamboleo, ukosefu wa haki msingi za binadamu pamoja na kufanyishwa kazi za suluba kwa ujira kiduchu pasi na haki. Mambo yote haya ni kutokana na ukosefu wa ushirikiano wa kimataifa, hali inayopelekea baadhi ya watu kujinufaisha kwa migongo ya maskini. Hapa kuna haja ya kudumisha utawala wa sheria, kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu sanjari na kumwilisha huruma inayokwenda pamoja na haki.

Migawanyo hii pia inajionesha katika nchi: tofauti kubwa kati ya miji na vijiji; kati ya watu ndani ya nchi moja; mambo ambayo wakati mwingine yanachochewa na ubaguzi wa rangi, woga usiokuwa na misingi, hali ya  kutovumiliana pamoja na ukosefu wa utawala wa sheria. Mambo yote haya yanahitaji maboresho makubwa katika mawasiliano, mahusiano na kuweza mataifa kujenga madaraja ya kukutana, ili kujenga umoja na mshikamano wa kweli licha ya kudumisha uhuru wa kila nchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.