2015-04-10 12:10:00

Kuna umuhimu wa kukuza majadiliano kati ya sanaa na imani


Kardinali Giafranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anabainisha kwamba, kuna umuhimu wa kukuza mchakato wa majadiliano kati ya sana ana imani na kwamba uzuri ni haki ya kila mtu hata kwa maskini na kwamba, Kanisa linaposhiriki katika Onesho la kila baada ya miaka miwili ni dhamana ya kidini, ili kuangalia yaliyopita, kupanga ya sasa na kujiwekea mikakati kwa siku za usoni. Kardinali Ravasi ameyasema haya, Alhamisi tarehe 9 Aprili 2015 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu ushiriki wa Vatican kwenye Onesho la 56 la Sanaa Kimataifa, huko mjini Venezia.

Watu hawana budi kufungua macho yao kuona hata kile pengine kwa macho ya kawaida hakiwezi kuonekana, ndiyo maana kauli mbiu inayoongoza onesho ili inajikita katika Maandiko Matakatifu, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu..” Onesho hili la Sanaa Takatifu litaanza kutimua vumbi kuanzia tarehe 9 Mei hadi tarehe 22 Novemba 2015, huko mjini Venezia. Kazi za wasaniii maarufu ambazo zimechaguliwa kutoka sehemu mbali mbali za dunia zitaoneshwa.

Bwana Micol Forti, mkurugenzi wa kazi za sanaa kutoka Makumbusho ya Vatican anasema wasanii watatu walioteuliwa kwa mwaka huu ni: Monika Bravo kutoka Colombia, ambaye anaonesha ufundi mkubwa unaofumbatwa katika simulizi kwa njia ya maneno na mvuto mkubwa wa teknolojia iliyotumika. Msanii wa pili ni Elpida Hadzi Vasileva kutoka Macedonia, kazi yake inaonesha ufundi mkubwa katika masuala ya sanaa unaowaalika watu kuangalia kazi ya Mungu katika sanaa. Msanii wa tatu ni Mario Macilau ambaye amepiga picha nzuri sana kutoka Msumbiji, alikozalia na anakofanyia kazi zake. Ni picha zinazonesha mateso na mahangaiko ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Sanaa hii ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya watoto sehemu mbali mbali za dunia.

Baraza la Kipapa la Utamaduni linabainisha kwamba, baada ya kushiriki katika onesho la kimataifa lililofanyika kunako mwaka 2013, limeamua kuendeleza mchakato wa majadiliano kati ya imani na sanaa katika medani za kimataifa; majadiliano kati ya Kanisa na Sanaa katika ulimwengu mamboleo na kwamba, kuna haja ya kupanua wigo kwa kushirikisha kazi za wasaniii wa Muziki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.