2015-04-09 15:35:00

Watawa wanapaswa kufundwa barabara ili kukabiliana na malimwengu!


Walezi wa maisha ya kitawa na kazi za kitume hawana budi kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kuwafunda watawa wa leo na kesho mintarafu moyo wa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake, kwa kujenga na kuimarisha mahusiano ya upendo na udugu kama kielelezo cha utume wa kinabii. Ni changamoto inayotolewa na Professa Michelina Tenace kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriani wakati akichangia mada kwenye kongamano la malezi kimataifa linaloendelea mjini Roma kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani.

Watawa watambue kwamba, wanatoka katika familia, tamaduni na jamii mbali mbali, hivyo wanachangamotishwa na Mama Kanisa kujenga udugu unaosimikwa katika maisha ya kiroho, jambo ambalo linahitaji majiundo makini: kiakili, kiroho, kimwili, kiutu, kijamii na kimaadili ili kufanana na mafundisho ya Yesu Kristo. Changamoto kubwa kwa watawa ni kuhakikisha kwamba, wanafundwa ili kuchuchumilia utakatifu wa maisha, ili waweze kujisikia kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo.

Kwa upande wake Padre Amedeo Cencini, kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Wasalesiani, amewataka walezi kuhakikisha kwamba, wanasoma alama za nyakati na kuwasaidia vijana wao kufundwa na mazingira kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Majiundo endelevu ni mwendelezo wa kila ambacho watawa wanakipata katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kujifunza kuendelea kujifunza kwa ajili ya sifa na utukufu wa Kristo na Kanisa lake. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuondokana nan woga usiokuwa na mashiko, ukakasi wa maisha na hali ya kudhaniana vibaya; mambo ambayo kimsingi yanawafanya watawa wengi kushindwa kuona ukweli wa maisha.

Washiriki wa kongamano hili wanaendelea kushirikishana mang’amuzi mbali mbali katika mchakato wa malezi na majiundo katika maisha ya kitawa na kazi za kitume kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni fursa pia ya kuuliza maswali kwa wawezeshaji wakuu, ili kuondoa kudukudu katika mchakato wa malezi endelevu katika maisha ya kitawa na kazi za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.