2015-04-09 09:53:00

Imarisheni Uekumene wa damu na Makanisa ya Mashariki!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo tarehe 12 Aprili 2015 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wananchi wa Armenia, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Karne moja, tangu yalipotokea madhulumu ya kidini nchini Armenia. Ibada hii itafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.Itakuwa ni fursa kwa ajili ya kuomba huruma ya Mungu katika ukweli na haki kama sehemu ya mchakato wa kuganga na kuponya madonda ya madhulumu, tayari kuanza hija ya upatanisho na amani kati ya Mataifa ambayo bado yanaendelea kuteseka kutokana na madhulumu haya.

Baba Mtakatifu ameyasema haya  Alhamisi, tarehe 9 Aprili 2015 alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa Sinodi ya Upatriaki wa Kanisa la Kikatoliki la Armenia, ambao wako hapa mjini Roma kushiriki katika tukio hili la kihistoria. Umati mkubwa wa Familia ya Mungu inayoishi uhamishoni itajiunga katika maadhimisho. Baba Mtakatifu anayakumbuka maeneo ambayo yalishambuliwa kiasi cha kutishia kutoweka kwa Wakristo.

Familia ya Mungu nchini Armenia kabla ya kuongokea Ukristo, ilikuwa na amana na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na kitamaduni, kiasi cha kuendelea kushikamana hata baada ya madhulumu na nyanyaso walizokumbana nazo, changamoto ya kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwawezesha kuwa waaminifu kwa Kristo hata walipokuwa wanakabiliana na magumu. Maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka mia moja ni kuangalia Fumbo la historia ya giza ambalo liliusonga moyo wa mwanadamu kiasi hata cha kupanga na hatimaye kusababisha mauaji ya kikatili kwa ndugu kwa kumhesabu kuwa ni adui bila hata kutambua utu wake.

Madhulumu haya anasema Baba Mtakatifu, yamewafungulia waamini mchakato wa kushiriki katika mateso yanayokomboa, jambo lililowapatia ujasiri kumuungama Kristo na Kanisa lake, kwa kumwaga damu yao na wengine kulazimika kuyakimbia makazi yao. Huu ni mwendelezo wa mateso ya Kristo lakini ndani mwake kuna mbegu ya Ufufuko wake. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuwaelimisha waamini walei kusoma historia kwa mwelekeo mpya, ili kuona mateso na ufufuko katika maisha. Matukio yaliyopita, yawawezeshe waamini kuwa na ujasiri wa kutangaza Injili ya Furaha kwa njia ya ushuhuda wa upendo.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanajikita katika majiundo makini na endelevu kwa Wakleri na Watawa, kwani hawa ni wadau wa kwanza kabisa katika mchakato wa Uinjilishaji; changamoto na mwaliko wa kuimarisha umoja na udugu ili kuendeleza maisha ya kisinodi katika Upatriaki huu. Baba Mtakatifu amewakumbuka baadhi ya viongozi wa Kanisa waliosimama kidete kulinda na kuwatetea wananchi wa Armenia dhidi ya mauaji, nyanyaso na dhuluma. Kwa namna ya pekee, Papa Benedikto XV aliyemwomba Sultan Mehmet V kusaidia kusitisha mchakato wa mauaji ya Wakristo, akawa kweli ni kiongozi aliyeonesha upendo wa pekee kwa Wakristo wa Makanisa ya Mashariki.

Papa Benedikto XV akaanzisha Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki, Taasisi ya Kipapa kwa ajili ya Makanisa Mashariki na kunako mwaka 1920 akawatangaza Mtakatifu Efrehemu na Siro kuwa ni kati ya Walimu wa Kanisa. Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ijayo yatakuwa ni kwa ajili ya kumbu kumbu pia ya Mtakatifu Gregori wa Narek. Baba Mtakatifu anaendelea kuhimiza majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika ushuhuda wa damu ya Wakristo huko Mashariki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.