2015-04-08 16:06:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Huruma ya Mungu


Mpendwa mwana wa Mungu, tuko tena pamoja tukiendeleza shamrashamra za Pasaka. Ni Dominika ya II ya Pasaka ambayo Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2000 tarehe 1 Mei wakati wa kumtangaza mjumbe wa Huruma ya Mungu, Sr. Faustina, kuwa Mtakatifu. aliiteua na kuitangaza Dominika hii kuwa Sikukuu ya Huruma ya Mungu.

Kanisa latukumbusha katika sikukuu hii kujiaandaa siku zote kupokea Huruma ya Mungu daima na msamaha wa adhabu tunazositahili kwa sababu tumetenda dhambi. Ndiyo kusema, Mama Kanisa katika sikukuu hii tangu siku ilipotangazwa na hata leo na baadaye hutoa Rehema kamili kwa wale wote wanaotimiza masharti yaliyowekwa, yaani kuungama ndani ya siku 20 kabla, kupokea Ekaristi Takatifu, kushiriki katika sala au ibada ya kuitukuza huruma ya Mungu Kanisani au mbele ya Sakramenti Kuu au mbele ya Tabernakulo, kusali kwa nia za Baba Mtakatifu (Nasadiki mara 1, Baba Yetu mara 1). Kwa jinsi hiyo ni lazima kila anayetaka kufaidi zawadi hii ya Rehema kamili awe katika hali ya neema ya utakaso wakati wa kukamilisha masharti hayo. Iwapo baadhi ya masharti hayakutimizwa, basi mtu huyo hujipatia Rehema isiyo kamili.

Mpendwa msikilizaji pengine mmoja aweza kuuliza hivi Rehema kamili na Rehema isiyo kamili ni nini? Kadiri ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 1471 hutueleza kuwa Rehema kamili ni msamaha wa adhabu zote za dhambi ambazo tulikwisha ungama. Rehema isiyo kamili ni msamaha wa sehemu tu ya adhabu hizo. Rehema kamili ni zawadi ambayo hutolewa na Kanisa kwa mtu anayetimiza masharti tajwa na kwa hakika Kanisa linapata kuchota zawadi hii toka katika kisima kile cha mastahili ya msalaba wa Kristo na toka mastahili ya Watakatifu wa mbinguni.

Mpendwa mwana wa Mungu, ni katika Dominika hii ya Huruma ya Mungu Mama Kanisa haachi kutuwekea Neno la Bwana linaloonesha jinsi wenzetu jumuiya ya kwanza ya Mitume pamoja na waamini wengine walivyokuwa wakiishi furaha ya ufufuko. Kumbe mwaliko toka Neno la Mungu ni kujibu swali hili: Ni kwa namna gani twaweza kudhihirisha kuwa Bwana amefufuka?

Katika somo la kwanza toka kitabu cha Matendo ya Mitume, mwandishi anatuonesha jinsi Waamini walivyokuwa na moyo wa umoja, yaani roho moja katika Kristu. Wanatangaza habari njema ya ufufuko kwa furaha. Ujumbe wao unaletwa mbele ya watu kwa nguvu, na hivi tunajiuliza nguvu hii walipata wapi?  Kwa hakika nguvu hii waliipata katika Kristo mfufuka na hasa katika kukubali kubadirisha maisha yao na kumfuasa Bwana mshindaji.

Waliweza kukusanya mali yao na kuiweka pamoja chini ya uongozi wa Mitume na hivi mzizi wa ubinafsi walijitahidi kuukata kwa namna hiyo, wakijikabidhi mikononi mwa Mungu kwa njia ya jumuiya yao. Kwa sababu hiyo kila mtu alipata mahitaji yake katika usawa, na furaha ya ufufuko ilizidi kupamba moto. Mpendwa msikilizaji, jambo la kuweka mali pamoja, kupendana kwa kujenga roho moja katika Bwana kuliwafanya Mitume pamoja na Waamii wengine waweze kueneza habari njema yakuwa Bwana amefufuka. Ni kwa jinsi hiyo mwandishi anataka kutufundisha nini maana ya jumuiya ya kikristu inayoongozwa na imani na upendo thabiti katika Kristu mfufuka. Anataka tuelewe kuwa kazi ya kimisionari ni kupendana na toka katika upendo tutaweza kuwahurumia na kuwahudumia wengine.

Aidha wito wetu leo hii ni kuitika na kutafakari vema mtindo huo wa maisha ya Jumuiya ya kwanza, yaani wa kuweka mali pamoja katika mwanga wa Neno la Mungu hasa katika hali ya ulimwengu wetu kwa sasa inayoonesha kuwa kuweka mali pamoja ni jambo ambalo haliwezekani! Uroho wa mali ni mkubwa kiasi kwamba unatisha! Nchi zetu zinaingia katika uchumi anguko si kwa sababu hatuna kitu bali tuna kitu kilichokatwakatwa vipande na kuingizwa katika mifuko mbalimbali ambayo wakaguzi wa hesabu za umma hawawezi kuifikia!

Mpendwa furaha ya ufufuko ndo hiyo? Je unawaza na kuwazua kujinasua katika mtego huu mkali unaozamisha jahazi nchi katika kilindi cha maji? Tafakari, hata hivyo jibu ni fupi tu, Hii si furaha ya Pasaka bali ni ufisadi dhidi ya pasaka! Ni kinyume na maisha mapya, maisha ya kujenga umoja kamili na Mungu, maisha ya ufufuko.

Madhulumu ya maisha mapya yanahitaji kukutana na nguvu mpya ambayo kwa hakika ni maisha ya huruma  na mapendo ya jirani katika jumuiya. Ndiyo kusema kuishi maisha mapya kadiri ya Dominika ya Huruma ya Mungu ni kuwaombea wanadamu wote hasa wakosefu ili watubu, tukiwa tunafahamu kuwa katika sikukuu hii milango ya rehema iko wazi na Mto wa rehema na Huruma ya Mungu unawaelekea watu wote na hasa wanyenyekevu. Kumbe, katika sikukuu hii tunaalikwa kutembelea wagonjwa, maskini na wafungwa, kwa kifupi kutenda matendo ya huruma kwa Wahitaji. Ni siku ya kumrudishia Mwenyezi Mungu shukrani kwa njia ya matendo yetu ya huruma.

Mpendwa msikilizaji, katika somo la pili Mtakatifu Yohane anatualika kutambua kuwa furaha ya kweli inakuja kwetu kwa njia ya kukiri kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu. Mungu aliyeshuka kwa sababu ya Huruma yake kwa mwanadamu. Na kwa namna hiyo yaani kwa njia ya imani nasi tunakuwa watoto wa Mungu. Imani ni tunda la ufufuko na tunda hili haliishii hewani bali lazima lizae matunda ndiyo upendo kwa wengine. Hali hii ya upendo inajionesha katika jumuiya ya Waamini wa kwanza chini ya Mitume yaani kumega mkate kwa pamoja.

Basi mpendwa maisha ya Jumuiya Ndogondogo katika majimbo yetu ni alama sahihi ya mapendo kwa jirani. Ndiyo kusema jumuiya ziwe ni vyombo vya upendo na mapatano ya familia ya Mungu. Kwa njia ya Mapendo katika jumuiya tutashinda mparaganyiko uliopo katika ulimwengu huu wa sasa. Ni kwa njia ya mapendo ya jirani tutadhihirisha imani yetu kama anavyotufundisha Mtume Yakobo.

Katika somo la Injili hali ya maisha ya jumuiya inajionesha wazi. Wanafunzi wa Bwana yaani Mitume wako pamoja ingawa wanahofu! Bwana anawakuta wakiwa pamoja na kuwatakieni amani. Anawaonesha alama za madonda na wanafurahi wakisema tumemwona Bwana! Ni katika jumuiya hiyo Bwana anawavuvia Roho Mtakatifu ili wapate kuondolea dhambi. Ni siku hii anaweka sakramenti ya kitubio katika Kanisa na kisha anawatuma wakaende kutangaza habari njema. Kumbe toba ni mlango wa kazi ya kimisionari, ni mlango wa imani, ni mlango wa wokovu. Analikabidhi kanisa ufunguo wa kufunga na kufungua katika mambo yamhusuyo Mungu katika uhusiano wake na mwanadamu. Ni katika kusanyiko la upendo kama hilo Bwana atawavuvia Roho Mtkatifu, ni katika kusanyiko hilo Bwana atawajalia taji la furaha, tumemwona Bwana na tumefurahi. Ndiyo kusema mpendwa msikilizaji furaha na mapendo ya Bwana yajidhirisha wazi daima katika maisha ya Jumuiya.

Jumuiya wakati fulani zinakuwa na watu walio na mashaka katika imani. Hali hii inajionesha leo kwa njia ya Mtume Tomasi ambaye hakuwapo pamoja na wenzake siku ya kwanza. Haamini na bado anamashaka kuhusu ufufuko! Siamini mpaka nitie vidole vyangu katika makovu ya Bwana! Baada ya siku nane Bwana anawatokea tena na Mt. Tomasi yupo. Bwana anamwambia lete mikono yako na uweke kidole chako katika ubavu wangu na usiwe asiyeamini! Tomasi anajibu, Bwana wangu na Mungu wangu! Mpendwa, Mtume Tomasi anapokiri udhaifu wake anatufundisha kuwa watu wa imani na unyenyekevu mkubwa na hivi baada ya ufufuko hakuna mashaka tena kinachobaki ni kwenda kutangaza habari ya furaha kwa mataifa.

Mpendwa leo hii wapo watu wa namna hii katika jumuiya zetu. Kumbe wanaalikwa na Bwana kusadiki pasipo kuona, na kwa namna hiyo Bwana anatangaza heri kwa wasioona wakasadiki na si kwa wanaosadiki kwa sababu ya kuona. Mwishoni mwa sehemu ya Injili ya Dominika hii, Mwinjili anatuaambia pia zipo ishara nyingi ambazo hazikuandikwa na hivi mtu asishangae ishara nyingine ambazo hazimo katika Biblia lakini ni muhimu kwa imani yetu na maisha ya Kanisa kwa ujumla.

Nakutakieni furaha tele katika kipindi chote cha Pasaka na Mungu azidi kuwa nawe, ukitekeleza mapenzi yake katika Jumuiya na uifanye Jumuiya yako iwe kama jumuiya ya kwanza ya Waamini. Tukutane tena Dominika ijayo.

Na Padre Richard Tiganya C.PP.S.  








All the contents on this site are copyrighted ©.