2015-04-08 12:17:00

Siku ya Kimataifa ya Waromania! Waheshimu, wao pia wameumbwa na Mungu


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya CCEE  kwa kushirikiana na Shirikisho la Makanisa ya Kiangalikani Barani Ulaya CEC, kwa pamoja yametoa ujumbe katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Waromania, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Aprili kwa kutambua kwamba, uwepo wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wanapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe wasibezwe wala kutwezwa kama inavyojionesha sehemu mbali mbali za Ulaya.

Ujumbe wa mshikamano na mapendo umetiwa mkwaju na Kardinali Peter Erdò, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE na Askofu Christopher Hill, Rais wa Shirikisho la Makanisa ya Kiangalikani Ulaya, CEC.Waromania ni watu ambao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe haijalishi lugha, tamaduni au mahali anapotoka mtu, jambo la msingi ni kwamba, ameumbwa kwa sira na mfano wa Mungu, hawa ndio wanaopaswa kutangaziwa Habari Njema ya Wokovu, kama Yesu mwenyewe anavyokazia kwa wanafunzi wake.

Kwa bahati mbaya, Waromani hawa ni watu ambao wanatengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi cha kujikuta wanatumbukizwa katika umaskini wa hali na kipato pamoja na nyanyaso mbali mbali. Licha ya madhulumu na mateso makali waliyokumbana nayo katika historia, bado ni watu wenye utajiri mkubwa katika maisha na tamaduni zao. Ni watu wanaothamini sana Injili ya maisha, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, upendo kwa watoto na imani kwa Mwenyezi Mungu. Wanaheshimu wafu wao na kupenda muziki ambao kwa asili uko katika vinasaba vya maisha yao.

Waromania wanapaswa kusaidiwa kuweza kuishi vyema na kushirikishwa kikamilifu katika mfungamano wa kijamii. Wasaidiwe kupata fursa za ajira na kwa upande wa Makanisa, wawahudumie kikamilifu katika maisha yao ya kiroho kwa kuwa na mikakati bora. Wapewe elimu itakayowakomboa katika umaskini na ujinga. Watendewe mema na kupewa haki zao msingi. Wakristo wawe ni mfano wa Msamaria mwema, kwa kutenda na kutekeleza yale ambayo Yesu anawatuma kufanya na kwa njia hii, kweli Wakristo watakuwa ni ndugu na jirani wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.